Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma Mhe. Peres Magiri, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara wilayani humo.
Amesema jumla ya kilomita 268 za barabara zimekarabatiwa kwa kiwango cha lami, ikiwa ni pamoja na barabara ya Mbamba Bay – Kilosa, ambapo kazi bado inaendelea katika kilomita 5.5.
Hata hivyo amesema Kwa maeneo yenye miinuko mikali, kilomita 1.2 ya barabara inajengwa kwa zege, huku madaraja 12 yakiwa tayari yamejengwa.
Ameongeza kuwa barabara ya kutoka Njambe hadi Ndonga yenye urefu wa kilomita 6.9, ambayo haikuwa inafikika tangu uhuru, sasa imefunguliwa na kwamba serikali imetumia shilingi bilioni 11.2 kuboresha barabara kupitia TARURA..
Akizungumzia barabara ya lami nzito kutoka Mbinga hadi Mbambabay Mkuu wa Wilaya amesema barabara hiyo iliyogharimu shilingi bilioni 129 imeifungua wilaya ya Nyasa.
Kabla ya ujenzi wa barabara hii, wananchi walilazimika kusafiri kwa zaidi ya saa saba hadi nane, hasa wakati wa mvua, ambapo safari ilikuwa ikichukua siku nzima.
Hata hivyo, kwa sasa safari hiyo inachukua saa moja na nusu, kutoka Mbambabay hadi Mbinga hali ambayo imerahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya ya Nyasa, Mhe. Starwat Nombo amesema barabara hizo zimekuwa mkombozi kwa wananchi kwa kuwa zimefungua milango ya fursa mbalimbali, zikiwemo za utalii katika mji wa Mbamba Bay na Mualo Bichi.
Mkazi wa Mbamba Bay, Bw. Andrea Ligola ameishukuru serikali kwa kuboresha barabara hizo, akieleza kuwa awali usafirishaji wa dagaa ulikuwa mgumu kutokana na magari kukwama na bidhaa kuharibika njiani.
Naye Emakulata Kayombo, mkazi wa Mbamba Bay, amepongeza juhudi za Rais Samia, akisema barabara hizo zimerahisisha usafirishaji wa mizigo na kuongeza idadi ya mabasi kutoka mawili hadi 12.
Maendeleo haya yanaonesha jinsi serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inavyowekeza katika miundombinu ili kuinua uchumi wa wananchi wa Nyasa na Tanzania kwa ujumla.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.