Katika hali ya hamasa kubwa, umati mkubwa wa wananchi wa Mji wa Songea mkoani Ruvuma umejitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Majimaji, kumshuhudia na kumsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 23 Septemba 2024, katika kilele cha Tamasha la Tatu la Kitaifa la Utamaduni lililoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo mkoani Ruvuma.
Mhe. Rais Dkt. Samia alikuwa mgeni rasmi wa tamasha hilo, ambalo limejikita katika kuonesha na kusherehekea utajiri wa urithi wa kitamaduni wa Tanzania. Katika hotuba yake, Rais Samia aliipongeza Wizara ya Utamaduni kwa juhudi zake za kuenzi na kulinda urithi wa kitamaduni, akisisitiza kuwa tamaduni ni nguzo muhimu katika kudumisha umoja wa kitaifa na utambulisho wa Watanzania.
Kabla ya kutoa hotuba yake, Rais Samia alitembelea mabanda ya maonesho ya utamaduni, ambapo alijionea kazi mbalimbali za sanaa na utamaduni, na hata kushiriki kucheza mchezo wa bao, jambo lililowafurahisha sana wananchi na wasanii waliokuwepo. Rais Samia aliwapongeza wasanii kwa kazi zao na kuwaahidi kuendeleza juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya sanaa na utamaduni nchini.
Aidha, katika hotuba yake, Mhe. Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kuhifadhi na kufundisha mila na desturi za kitanzania kwa kizazi kijacho. Alieleza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya utamaduni na sanaa, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya maeneo ya kihistoria kama vile Uwanja wa Majimaji, ambao una umuhimu mkubwa kwa historia ya Tanzania.
Rais Samia pia aliwataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kuhifadhi mazingira, hasa maeneo yenye urithi wa kitamaduni, akibainisha kwamba urithi huu ni rasilimali isiyoweza kurejeshwa mara inapoharibika. Aliwaasa Watanzania kuenzi na kuthamini utamaduni wao kwa kuhakikisha kuwa mila, desturi na lugha zetu za asili zinaendelea kudumishwa.
Shughuli hiyo inaendelea kwa shamrashamra, huku wananchi wakionesha shauku na furaha kubwa kwa ziara ya Rais Samia katika eneo hilo lenye umuhimu mkubwa kwa historia na utamaduni wa taifa
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.