RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 40 kwa ajili ya kutekelezaji miradi mbalimbali katika sekta ya elimu mkoani Ruvuma.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas wakati anatoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa CCM kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2022 na Januari hadi Juni 2023 kwenye ukumbi wa Parokia ya Bombambili mjini Songea.
Akizungumzia sekta ya elimu Kanali Thomas amesema katika kipindi hicho sekta ya elimu ilipokea shilingi bilioni 7.7 kujenga shule mpya za sekondari katika Halmashauri zote nane zilizopo mkoani Ruvuma
“Ujenzi huu unajumuisha shule za sekondari za kata kumi zilizogharimu shilingi bilioni 4.7,shule ya sekondari mpya ya wasichana ya Mkoa iliyopewa jina la Dkt.Samia Suluhu Hassan iliyojengwa wilayani Namtumbo kwa gharama ya shilingi bilioni 4.1’’,alisema.
Ameongeza kuwa sekta ya elimu pia ilipokea fedha za ujenzi wa mabweni saba ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa gharama ya shilingi milioni 640 na ujenzi wa vyumba vya madarasa 792 vya elimu ya msingi na sekondari vilivyogharimu shilingi bilioni 14.93.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa,Rais Samia pia katika sekta ya elimu ametoa shilingi milioni 250 kujenga shule mpya ya msingi katika kitongoji cha Lizaboni Halmashauri ya wilaya ya Songea.
Ameongeza kuwa serikali imetoa fedha zaidi ya shilingi bilioni mbili kukamilisha vyumba vya madarasa 121 vya shule za msingi na sekondari Pamoja na maabara 23 za shule za sekondari kupitia fedha za Tozo na Serikali Kuu.
Kulingana na Mkuu wa Mkoa,katika sekta ya elimu Rais Samia pia ametoa shilingi bilioni 3.12 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 156 vya madarasa katika shule za sekondari mkoani Ruvuma hali iliyosababisha kuondoa kabisa tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa.
Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa walimu wote wa shule za msingi na sekondari wapatao 9,079 katika Mkoa wa Ruvuma wamegawiwa vishikwambi kwa ajili ya uboreshaji wa ufundishaji.
Mkoa wa Ruvuma una jumla ya shule za msingi 841 na shule za sekondari 233
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.