Na Albano Midelo,Songea
Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Dkt.Frank Walter Steinmeier amewafariji wahanga wa tukio la vifo vya mashujaa 67 waliua kikatili na wakoloni wa Kijerumani miaka 117 iliyopita mjini Songea mkoani Ruvuma.
Wakoloni wa kijerumani waliwauawa kikatili kwa kuwanyonga mashujaa wa vita ya Majimaji wapatao 67 wakiongozwa na Jemedari wa kabila ya wangoni Nduna Songea Mbano mwaka 1906 kisha kuwazika katika makaburi mawili ndani ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea.
Akizungumza baada ya kutembelea Makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea na kuzungumza na wahanga wa tukio hilo,Rais wa Ujerumani Dkt.Steinmeier amesema baada ya matukio ya vifo vya watu 67 yaliyotokea hapa Songea miaka 117 iliyopita,yeye kama Rais wa Ujerumani amepata fursa ya kukutana na wahanga kwenye eneo la tukio na kuwaomba msamaha kwa kilichotokea.
Amesema ameguswa na historia ya shujaa wa wangoni Nduna Songea Mbano na mashujaa wengine 66 ambao amesema historia yao ni ya kuhuzunisha sana hasa vifo vyao ambavyo waliuawa kikatili kwa kunyongwa.
“Leo baada ya kufika hapa Songea nimefahamu kuhusu jambo la kinyama walilotendewa mashujaa hawa limeendelea kuathiri familia nyingi hadi leo,ni watu wachache sana wanaofahamu historia hii nchini Ujerumani’’,alisisitiza Rais wa Ujerumani.
Amesema Mji wa Songea unawakilisha upinzani wa watanzania dhidi ya ukoloni wa kijerumani na kuongeza kuwa amefika Songea ili kubeba historia hiyo na kuipeleka kwa wajerumani wengi atakaporejea nchini kwake.
Hata hivyo amesema matukio yaliyotokea Songea miaka 117 iliyopita ni matukio yanayohusu jamii za nchi mbili za Tanzania na Ujerumani ambapo amesisitiza kuwa nchi ya Ujerumani lazima iwajibike kuhusu historia ya vita ya Majimaji ili kujenga kwa Pamoja Maisha ya siku za usoni.
Amemtaja Jemadari wa wangoni Songea Mbano kuwa alikuwa kiongozi shupavu katika vita ya Majimaji dhidi ya ukoloni wa kijerumani waliotawala kwa ukatili mkubwa.
Amesema baada ya kuzungumza na familia ya Songea Mbano ameguswa na mambo yote aliyoelezwa,waliyoyafanya majeshi ya wakoloni wa kijerumani.
“Mimi kama Rais wa Ujerumani naomba msamaha kwa mambo yote ambayo wajerumani waliwatendea mabibi na mababu zenu miaka 117 iliyopita,nawahakikishia kwamba sisi wajerumani tutajitahidi kupata majibu ya maswali yote ambayo hayana majibu na ambayo hayawapi amani’’,alisisitiza Dkt. Steinmeier.
Akizungumzia kuhusu masalia ya watu waliouawa miaka 117 iliyopita Rais huyo amesema masalia hayo kutoka Afrika Mashariki yalisafirishwa hadi nchini Ujerumani na kuhifadhiwa katika makumbusho na hifadhi za kiatropolojia ambako kuna maelfu ya mafuvu ya vichwa vya binadamu.
Amesema serikali ya Ujerumani inaendelea na jitihada za kutafuta fuvu la kichwa cha shujaa Songea Mbanonchini Ujerumani ambapo ameitaja changamoto kubwailiyopo ni kupima na kutambua masalia halisi ya binadamu kwa fuvu la mlengwa.
Hata hivyo amesema Tanzania na Ujerumani ni nchi ambazo zinaunganishwa na mambo mengi ikiwemo miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa.
Ameongeza kuwa Tanzania na Ujerumani pia zimeunganishwa na historia ya mashujaa wa Majimajiambapo amesema mwakani Ujerumani inatarajia kufanya maonesho na Makumbusho ya Taifa ya Tanzania.
Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii amempongeza Rais wa Ujerumani kwa kutembelea Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea ambapo amesema hilo ni tukio la kihistoria kwa Rais wa Ujerumani kutembelea makumbusho hiyo.
Amesema serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ipo tayari kutumia historia ya vita ya Majimaji kwa faida ya kijamii na kiuchumi kwa nchi za Tanzania na Ujerumani
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Mbunge wa Songea mjini ambaye pia ni Waziri waUtamaduni,Sanaa na Michezo,Dkt.Damas Ndumbaroamesema nchi za Tanzania na Ujerumani zinapaswa kutengeneza mahusiano na ushirikiano mzuri na kusahau yaliyopita kwenye vita ya Majimaji.
Ametoa rai kwa nchi zote mbili kushirikiana na kuleta maendeleo katika mji wa Songea na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla ambapo alisisitiza wananchi wa Songeakuona makumbusho ya kisasa kati ya Ujerumani na Songea yakijengwa mjini Songea.
Amesema ziara ya Rais wa Ujerumani mjini Songea nihatua muhimu sana ya kuleta maridhiano na mahusiano mazuri ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi hizo .
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.