MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amezindua Baraza la Wazee Mkoa wa Ruvuma katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Songea Klabu.
Akizungumza kabla ya uzinduzi huo,Kanali Thomas amesema serikali imekuwa ikitoa huduma kwa wazee kwa kuzingatia sera ya Taifa ya wazee ya m waka 2003 na Sera ya Afya ya mwaka 2007, sanjari na miongozo mbalimbali ili kuhakikisha wazee wanastawi vyema bila kubaguliwa.
“Sote tunafahamu suala la uzee na kuzeeka limekuwa lenye umhimu mkubwa kwa Taifa hasa kuhusiana na mitazamo ya kiuchumi,kisiasa na kijamii’’,alisisitiza Kanali Thomas.
Hata hivyo amesema wazee ni moja ya kundi lilikuwa limetengwa katika jamii hivyo nguvu za ziada kutoka serikalini na wadau kwa ujumla zimeendelea kufanyika ili kuhakikisha wazee wanapata haki zao za msingi.
Mkuu wa Mkoa amesema tayari Mkoa umewatambua wazee katika ngazi zote ambapo jumla ya wazee 96,054 walitambuliwa katika Mkoa kwa lengo la kuhakikisha wanapatiwa huduma muhimu zikiwemo matibabu bure.
Amesema uundaji wa mabaraza ya wazee umefanyika katika Halmashauri zote nane ambapo takwimu zinaonesha kuwa yameundwa mabaraza katika kata 173,vijiji na mitaa 686 ,Halmashauri nane na Baraza la wazee la Mkoa ambalo linazinduliwa leo.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Ruvuma Viktor Nyenza akitoa taarifa ya huduma ya wazee amesema jumla ya wazee 43,312 wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bure saw ana asilimia 45 na wazee 5,384 wananufaika na huduma za bima ya afya.
Nyenza amesema Mkoa unasimamia utoaji na upatikanaji wa huduma bora za matibabu bila malipo kwa wazee wote kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vinavyomilikiwa na serikali.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Ruvuma Ezieli Nyoni akizungumza kwa niaba wazee mara baada ya uzinduzi wa Baraza hilo,amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuzindua Baraza hilo ambalo liliundwa Juni 2021.
Amesema sasa Baraza limepata nguvu na lipo tayari kuanza kazi ya kuwatumika wazee hasa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee.
Amezitaja baadhi ya changamoto za wazee kuwa ni upungufu wa baadhi ya bidhaa za afya kwa ajili ya matibabu ya wazee,umasikini na hali duni kiuchumi kwa wazee na uwepo wa Imani potofu za kishirikina zinazotishia usalama wa wazee katika baadhi ya maeneo.
Kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012,idadi ya wazee Tanzania imeongezeka kufikia milioni 3.1 ukilinganisha na wazee milioni 1.4 mwaka 2002.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma
Septemba 3,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.