MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Songea kuhakikisha ujenzi wa wodi tatu za hospitali ya wilaya hiyo unakamilika ndani ya mkataba ili wananchi waanze kupata huduma mapema.
RC Ibuge ametoa agizo hilo baada ya kukagua mradi huo ambao serikali imetoa shilingi milioni 500 kutekeleza mradi huo ambao ujenzi wake umeanza Mei 23 mwaka huu na unatarajia kukamilika Novemba mwaka huu.
“Naagiza twende kwa spidi lakini kazi iwe yenye ubora,mimi ninapofanya ziara huwa sitoi taarifa,nitarudi wakati wowote,nikikuta jengo halina ubora,nitabomoa kwa gharama yako’’,alisisitiza Brigedia Jenerali Ibuge.
Kabla ya kukagua mradi huo,RC Ibuge alikagua majengo saba ya hospitali ya wilaya ya Songea ambayo yamejengwa katika kijiji cha Mpitimbi na kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.8 ambapo ameagiza majengo yote yaanze kutoa huduma ikiwemo huduma ya upasuaji.
RC Ibuge amesema serikali imetumia gharama kubwa kujenga majengo ya hospitali hiyo,ambapo amesisitiza yasipotumika itakuwa sawa na kazi bure hivyo amewaomba madiwani wa Halmashauri hiyo,kushirikiana ili kuhakikisha hospitali hiyo inaanza kutoa huduma za afya mapema.
Awali akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Dr.Gofrey Kihaule amesema serikali ilitoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa hospitali hiyo ambapo mradi ulianza kwa majengo saba.
Ameyataja majengo hayo kuwa ni majengo ya wagonjwa wa nje (OPD),utawala,mionzi ,kufulia,bohari ya dawa na jengo la upasuaji ambalo linahusisha mama na mtoto na kwamba ujenzi uliendelea mwaka 2020 ambapo serikali ilitoa shilingi milioni 300 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi ikiwemo ujenzi wa njia za kupitishia wagonjwa.
Hata hivyo Dr.Kihaule amesema ujenzi wa hopsitali hiyo ulikamilika Julai 2020 ambapo huduma za matibabu kwa wagonjwa wa nje zilianza kutolewa rasmi na kwamba katika bajeti ya mwaka 2020/2021 Halmashauri imepokea milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi tatu ambazo ni wodi ya watoto,wanawake na wanaume.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Juni pili,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.