MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema amedhamiria kuimarisha usimamizi, ulinzi na uhifadhi Maliasili kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Ibuge amesema Mkoa umekuwa katika mstari wa mbele katika kuwahamasisha wananchi juu ya utunzaji wa mazingira kwa kutokuchoma misitu hovyo na upandaji wa miti katika maeneo yaliyo wazi na kwenye vyanzo vya maji.
Hata hivyo Ibuge amesema Mkoa wa Ruvuma unalengo la kupanda miti ya biashara eka 100,000 na kwamba Mradi huu unatekelezwa kwa kupanda miti maeneo ya serikali kuu, serikali za mitaa, mashuleni pamoja na vijijini.
RC Ibuge amesema Mkoa una mpango wa kuanzisha mashamba ya wanyamapori kwenye jumuiya tano, Kisiwa cha Lundo pamoja na chuo cha Maliasili cha Likuyusekamaganga ili wananchi wajifunze toka hapo na kuanzisha mashamba binafsi.
Ameishukuru serikali kwa kuboresha miundombinu ya barabara na anga na hivyo kuufungua Mkoa na kuchochea shughuli za maendeleo ikiwemo utalii.
‘’Mkoa kwa kushirikiana na WWF tumeandaa mpango wa kukuza Utalii, kutengeneza filamu fupi ya matangazo, vipeperushi pamoja na jarida la kuonyesha vivutio vya Mkoa ’’,amesema Brigedia Jenerali Ibuge.
Hata hivyo Ibuge amesisitiza kuwa baada ya Mkoa kubaini kuna vyanzo vya maji vinaharibiwa na shughuli mbalimbali za wananchi,ameutaja mpango uliopo sasa ni kuhakikisha kuwa vyanzo vyote vya maji vinakabidhiwa kwa Wakala wa Misitu TFS ili viweze kupimwa, kuwekewa mipaka pamoja na kupanda miti kwenye vyanzo vya maji.
Imeandaliwa na Bahati Nyoni
Kutoka Ofisi ya Habari ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma
Februari,8 2022.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.