MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewataka walimu na wadau wa elimu waweke msingi wa utawala bora kwenye maeneo ya shule.
Akizungumza katika kikao cha tathmini elimu klichofanyika kwenye ukumbi wa Songea Girls,amesema anayo nia, kiu na malengo ya kuhakikisha sekta ya Elimu Mkoani Ruvuma inapata maendeleo yanayostahiki.
Amesema ni wajibu wa Bodi na walimu kuweka mikakati ya ushirikishwaji wa wadau kwenye ngazi ya shule pamoja na kuweka mikutano ya wazi na wazazi kwani huo ni utawala bora ili kupanga maendeleo ya shule.
‘’Ndugu wadau wa Elimu tathmini ya utekelezaji wa kazi ni kipimo muhimu cha ufanisi wa shughuli yoyote kwasababu tukifanya tathmini tunaweza kubaini mafanikio na changamoto hivyo inakuwa rahisi kuzitatua’’, amesema RC Ibuge.
Aidha, amesisitiza wazazi wawajibike ipasavyo ili kutatua tatizo la upungufu wa chakula na lishe mashuleni kwani huwezesha watoto kuwa na afya nzuri, hupunguza utoro, huongeza usikivu na kuboresha afya na huinua kiwango cha ufaulu.
RC Ibuge ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kushiriki zoezi la uandikishaji wa anwani za makazi na sense ya watu inayotarajia kufanyika Agosti 2022.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stephen Ndaki amesema Mkoa una jumla ya shule 1039 ambapo shule za msingi zipo 823 na sekondari zipo 216, pia una jumla ya wanafunzi 465,334 kati ya hao shule ya msingi zina wanafuzi 390,855 na sekondari 74,479.
Ameitaja hali ya ufaulu kwa mwaka 2019 ulikuwa asilimia 83.7 na 73.1 kwa shule za msingi hadi kidato cha nne na kwa kidato cha tano ufaulu ulikuwa asilimia 86.6 kwa mwaka 2019 na asilimia 91.1 kwa mwaka 2021.
Kauli Mbiu ya Elimu katika Mkoa wa Ruvuma ni ‘’Umoja wetu kwa Maendeleo ya Elimu yetu’’.
Imeandaliwa na Bahati Nyoni
Kutoka Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Machi 29 2022.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.