Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameviagiza vyombo vyote vya usafirishaji abiria yakiwemo malori,kuhakikisha wanaweka vipukusa mikono(sanitizers) ili kupunguza maambukizi ya UVIKO 19.
RC Ibuge ametoa maagizo hayo wakati anafunga kikao cha wadau wa usafiri na usafirishaji kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea ambapo pia yamepitishwa maazimio ambayo yanahitaji utekelezaji wa pamoja.
Maazimio na maelekezo mengine ni lazima abiria wote wavae barakoa ambapo RC Ibuge amesisitiza ni lazima kila mmoja kulinda afya yake na ni wajibu wa kumlinda mwingine dhidi ya UVIKO 19.
“Ukikiuka kumlinda mwingine maana yake umevunja sheria na ni kosa la jinai ambalo halina tofauti na kukusudia kuua kwa hiyo sio hiari,unapopanda chombo cha moto uhakikishe una barakoa’’,alisisitiza Ibuge.
Mkuu wa Mkoa pia ameagiza kila stendi ya mabai ziwekwe ndoo za kutosha zenye maji tiririka na sabuni kwenye maeneo muhimu ya kuingilia na kutoka magari na yeyote ambaye anakiuka afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Ameagiza elimu endelevu ya kukabiliana na UVIKO 19 itolewe na wataalam wa afya kupitia redio za kijamii zilizopo mkoani Ruvuma ili wananchi wapate uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa huo.
Hata hivyo amesema stendi ya Mfaranyaki mjini Songea isitumike kubeba abiria kwa sababu ya kuwepo kwa kituo cha mafuta ambacho kinaweza kusababisha maafa makubwa kwa wananchi likitokea tatizo kama moto
Akizungumzia utekelezaji wa sheria ya abiria kufunga mikanda na abiria wote kukaa kwenye viti bila kusimamishwa,Brigedia Jenerali Ibuge amesema ni muhimu kuzingatia sheria ili kupunguza msongamano kwenye vyombo vya abiria hivyo kupunguza maambukizi.
Kuhusu madereva bodaboda kubeba abiria zaidi ya mmoja,Mkuu wa Mkoa amesema suala hilo halina mjadala ni marufuku kubeba mishikaki na kwamba kofia kwa abiria ni lazima ili kujikinga.
Ametoa rai kwa wananchi wote mkoani Ruvuma kuchanja chanjo ya UVIKO 19,hata hivyo amesema chanjo hiyo ni hiari na kwamba chanjo hiyo imethibitika kitaalam inasaidia kushitua kinga ya mwili kukabiliana na UVIKO 19 hivyo kupunguza vifo au mgonjwa kuzidiwa hadi kuwekewa gasi ya kupumlia.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Agosti 6,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.