Wilaya ya Namtumbo inavyotekeleza miradi miwili ya maji yenye thamani ya zaidi ya sh.bilioni mbili na milioni 670
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amekagua miradi miwili ya maji ya Mkongogulioni na Milonji kata ya Lusewa wilayani Namtumbo inayotekelezwa na serikali kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni mbili na milioni 670.
Akitoa taarifa ya mradi wa maji wa Milonji Kata ya Lusewa,Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Namtumbo David Mkondya amesema mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 612.
Hata hivyo amesema mradi huo chanzo chake ni kisima kirefu na maji yake yanasukumwa kwa nguvu za jenereta na kwamba mradi unatekelezwa na Mkandarasi BERAS INVESTMENT LTD kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 ambao unatarajia kuhudumia watu 4988 katika kijiji cha Milonji.
Hata hivyo Mkondya amesema mradi huo unakabiliwa na changamoto za mwamko mdogo wa wananchi katika uchangiaji wa mfuko wa maji na kwamba RUWASA wilaya ya Namtumbo inaendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuchangia mfuko wa maji na kufanya ufuatiliaji na usimamizi kwa jumuiya ya watumiaji maji.
“Tangu mradi umekamilika mwaka 2015, kwa miaka mitano wananchi walikuwa wanakataa kuchangia mfuko wa maji kwa ajili ya mafuta ya jenereta hali iliyababisha kuendelea kutumia maji ya mtoni na visima ambayo sio safi na salama ‘’,alisema Mkondya.
Akizungumzia mradi wa maji ya Mkongogulioni na Nahimba,Kaimu Meneja wa RUWASA amesema mkataba wa mradi huo unagharimu zaidi ya shilingi bilioni mbili na ulitarajiwa kukamilika Februari mwaka huu chini ya Mkandarasi Kipera Contructors LTD.
Amezitaja kazi ambazo zimepangwa kufanyika kulingana na mkataba kuwa ni ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 25,000 katika kijiji cha Nahimba,ukarabati wa matanki mawili moja likiwa na ujazo wa lita 150,000 katika kijiji cha Mkongo na lingine lita 25,000 katika kijiji cha Nahimba.
Kazi nyingine zinazofanyika kwenye mradi huo ni uchimbaji wa mitaro ya maji laini kuu urefu wa kilometa 15 na laini ya usambazaji kilometa 17.84,ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 46 ambapo baadhi ya maeneo yameanza kupata huduma ya maji ikiwemo kitongoji cha Litete kata ya Mkongogulioni.
Amezitaja kazi ambazo zinaendelea katika mradi huo kuwa ni ulazaji wa mtandao mpya wa usambazaji maji katika kijiji cha Mkongogulioni ambapo mradi huo hivi sasa unakamilishwa na RUWASA kwa njia ya force akaunti,baada ya Mkandarasi kuchelewa kukamilisha na kwamba utekelezaji wake umefikia asilimia 85 na huduma ya maji imeanza kutolewa baadhi ya maeneo.
Akizunguma mara baada ya kukagua miradi hiyo ya maji,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema amesikitishwa na wananchi wa kijiji cha Milonji kushindwa kutumia maji tangu mradi ulipokamilika mwaka 2015 badala yake wananchi wameanza kutumia maji mwaka 2020.
“Watu 5000 katika kijiji cha Milonji wamekuwa hawapati maji kwa miaka mitano kwa sababu ya kuvutana,elimu ya umuhimu wa kuchangia maji imetolewa kwa miaka mitano,somo halikueleweka, anayepata shida ni mama na watoto ambao wanasafiri umbali mrefu kuchota maji’’,alisema Mndeme.
Amesema serikali ya Rais Magufuli katika Mkoa wa Ruvuma imetoa shilingi bilioni 30 za kuboresha sekta ya maji katika na kwamba kati ya fedha hizo,wilaya ya Namtumbo pekee imepokea zaidi ya bilioni 13 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji.
Ili kukabiliana na changamoto ya jenerata la kusukuma maji katika mradi huo,Mndeme amesema serikali mwaka huu inatarajia kufikisha umeme wa REA katika vijiji vyote ambavyo havijapata huduma hiyo,kikiwemo kijiji cha Milonji.
Mkuu wa Mkoa amewaasa wananchi hao kuendelea kuchangia kiasi cha shilingi 50 kila kaya kwa ndoo kwa ajili ya kununua mafuta ya kusukuma maji na kupata lita laki moja kwenye tanki kwa ajili ya matumizi ya wananchi katika kipindi hiki cha mpito wakati wanasubiri umeme wa TANESCO.
Akizungumza na wananchi wa mradi wa maji ya Mkongogulioni, Mndeme amesema serikali iliamua kumnyan’anya Mkandarasi kazi mradi huo kutokana na kuuchelewesha na kuamua ujengwe kwa nguvu za wananchi kwa kutumia force akaunti.
Vijiji vya Kata ya Mkongogulioni na Milonji kata ya Lusewa wilayani Namtumbo havijawahi kupata maji safi na salama ya bomba tangu nchi kupata uhuru mwaka 1961.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 6,Namtumbo
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.