Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ametoa rai kwa waumini kuendelea kuliombea Taifa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu ili uweze kufanyika kwa amani na utulivu.
Mndeme ametoa rai Jumapili hii aliposhiriki Ibada na waumini wa Kanisa Anglikana Mtakatifu Nicholaus lililopo mjini Songea.
Mkuu wa Mkoa ambaye pia amechangia Ujenzi wa Nyumba ya Mchungaji saruji tani tatu yenye thamani ya zaidi ya shilingi 900,000,amewashukuru waumini wote kwa kuliombea Taifa la Tanzania kuanzia kipindi cha corona na hata kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu ambao unatarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.
“Ndugu zangu nianze kuwashukuru kwa maombi yenu mnayoliombea Taifa hili,mkimuombea Rais wetu, mkiwaombea Mawaziri na viongozi wote wenye mamlaka katika nchi hii tunawashukuru sana maombi yenu yameifanya nchi yetu kuendelea kuwa na amani’’,alisema.
Hata hivyo Mndeme amesema umebaki muda mchache kuelekea Uchaguzi Mkuu hivyo amewaomba waumini kuendelea kuliombea Taifa la Tanzania ili Mwenyezi Mungu ausimamie uchaguzi ufanyike kwa amani na nchi iendelee kuwa kisiwa cha amani.
“Ndugu zangu tarehe 28 mwezi huu, Taifa letu la Tanzania linataingia katika uchaguzi mkuu wa Rais ,wabunge na Madiwani, Niwaombe,naomba tujitokeze kwa wingi ili tukachagua viongozi wapenda maendeleo watakaoliongoza Taifa hili katika kipindi kingine cha miaka mitano’’,alisema Mndeme.
Mndeme amewasisitiza Watanzania ifikapo Oktoba 28 kila mmoja achukue maamuzi sahihi kuchagua viongozi sahihi na wanaopenda maendeleo na nchi ya Tanzania iendelee kuimarika katika Nyanja zote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ushirika wa Mama wa Kristo (UMAKI) katika Kanisa la Anglikana Agnes Hinjo, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuja kuabudu katika ibada hiyo na kumuahidi kwamba wataendelea na maombi ya kuliombea Taifa la Tanzania siku zote.
“Sisi waumini wa Kanisa la Anglikana tupo kwenye maombi,UMAKI tumeamua kuchukua hatua za kuendelea na maombi tangu aliposema Rais Magufuli tufunge kwa ajili ya corona,hatujaacha,tupo kwenye maombi kwa ajili ya uchaguzi’’,alisema Hinjo.
Naye Mchungaji wa Kiongozi wa Kanisa hilo Padre Mathayo Chanangula katika mahubilri yake kwenye ibada hiyo amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kazi njema anayofanya ya kusimamia masuala ya kimwili na kiroho.
Padre Chanangula amesema msaada wa saruji ambao ameutoa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mchungaji utasaidia sana katika ukamilishaji wa nyumba hiyo ambayo itamwezesha Mchungaji kufanya kazi za kiroho kwa ufanisi zaidi.
Imeandaliwa na Aneth Ndonde
Kutoka ofisi ya Habari ya Mkoa wa Ruvuma
Oktoba 18,2020.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.