MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amezipongeza halmashauri sita kati ya nane zilizopata hati safi mkoani Ruvuma.
Mndeme ametoa pongezi hizo wakati anazungumza katika kikao kazi cha majumuisho cha kujadili taarifa ya CAG kuhusu hoja na mapendekezo ya Hesabu za serikali kwa mwaka 2018/2019 kilichofanyika Ikulu ndogo mjini Songea.
Kikao hicho kilijumuisha wakurugenzi wa Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma,wakuu wa wilaya zote tano,makatibu tawala wote na watalam ngazi ya Halmashauri na Mkoa.
Mndeme amezitaja Halmashauri ambazo zimepata hati safi kwa miaka mitatu na miaka minne mfululizo kuwa ni Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru,Halmashauri ya Namtumbo,Madaba,Nyasa,Halmashauri ya Mji Mbinga na Halmashauri ya Wilaya ya Songea,
“Kwa Halmashauri mbili za Manispaa ya Songea na Halmashauri ya Wilaya ya Songea zilizopata hati zenye mashaka,tunazielekeza zijipange upya na kuhakikisha ukaguzi wa 2019/2020 zinapata hati safi’’,alisisitiza.
Mkuu wa Mkoa amesisitiza kuwa hati zenye mashaka na hati chafu hazikubaliki katika Mkoa wa Ruvuma ambapo ameagiza wote waliosababisha kupatikana kwa hati hizo wanatakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu ili kuhakikisha kuwa kila mmoja anawajibika katika matumizi sahihi ya fedha za umma na kuzuia hoja.
Katika ukaguzi wa CAG katika kipindi hicho kwa Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma kulikuwa na hoja na mapendekezo 496 ya miaka ya nyuma ambayo yalikuwa hayajafungwa.
Hata hivyo Mndeme amesema hadi kufikia Machi mwaka huu baada ya zoezi la uhakiki kufanyika kiasi cha hoja na mapendekezo 240 yamefungwa na kubakiza 256 ambayo bado yanaendelea kufanyiwa kazi kwa kupeleka vielelezo kwa ajili ya uhakiki.
Katika kikao hicho cha majumuishi wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma walitoa taarifa kuhusu hatua ambazo wamezichukua kwa watumishi waliosababisha hoja zikiwemo watumishi hao kuwapa onyo la mdomo na onyo la maandishi.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 19,2020
Ikulu Ndogo Songea
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.