SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na wanawake katika ujenzi wa Taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme katika maadhimisho ya kilele ya siku ya wanawake Duniani Mkoani Ruvuma yaliyofanyika katika kijiji cha Kalanje wilayani Tunduru.
Mndeme amesema kutokana na serikali kutambua umuhimu wa wanawake imeziagiza Halmashauri zote kutenga asilimia nne ya mapato yake ya ndani kwa lengo kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2020 hadi Februari 2021 katika Mkoa wa Ruvuma,serikali imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 444,167,441.82 kwa vikundi 603 vya wanawake,vikundi 221 vya vijana na vikundi 203 vya watu wenye ulemavu.
“Mh.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatekeleza kauli mbiu hii ya Wanawake katika uongozi chachu kufikia dunia yenye usawa hivyo kwa vitendo, tunaona wakuu wa Mikoa/Mawaziri,wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi na wakuu wa Idara ambao ni wanawake ni jukumu letu kuwapa wanawake nafasi ya uongozi”,alisisitiza Mndeme.
Mndeme ameitaja siku ya wanawake kuwa ni muhimu sana kwa sababu inaonesha nafasi kubwa waliyonayo wanawake katika jamii yetu na katika uongozi na kutoa mchango mkubwa wa malezi ya watoto.
Amesema wanawake ni nguzo kubwa katika nchi kwa sababu wanatoa dira na mwelekeo wa maendeleo katika ngazi zote za kifamilia hadi uongozi wa juu ya nchi.
Awali Afisa maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Ruvuma Zawadi Nyoni akitoa historia fupi ya siku ya wanawake duniani amesema ilianzishwa mwaka 1900 kufuatia maandamano ya wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda nchini Marekani kupinga mazingira duni ya kazi.
Nyoni amesema wanawake walipinga ukosefu wa huduma za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji katika ajira ikiwemo wanawake kulipwa mshahara mdogo kwa kazi sawa ukilinganisha na wanaume.
Hata hivyo amewapongeza wanawake wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuwa mstari wa mbele katika Nyanja za kuleta maendeleo endelevu kwa Jamii ikiwemo kushiriki na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Amesema wanawake wamekuwa mstari wa mbele kulaani vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake na watoto hususani wa kike,kupinga matumizi ya dawa za kulevya,na kupambana na janga la UKIMWI na magonjwa ya mlipuko kwa kutumia elimu kwa jamii kwa njia ya sanaa.
kauli mbiu ya siku ya wanawake duniani mwaka huu ni Wanawake katika uongozi chachu ya kufikia dunia yenye usawa.
Imeandaliwa na Aneth Ndonde
Afisa Habari Halmashauri ya Madaba
Machi,9,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.