Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewaagiza watendaji katika Halmashauri ya Nyasa kuhakikisha wanabuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza ukusanyaji mapato.
Kanali Thomas ametoa agizo hilo wakati anazungumza na watumishi,madiwani na wazee wa Wilaya ya Nyasa kwenye ukumbi wa chuo cha VETA mjini Mbambabay.
Mkuu wa Mkoa ameitaja wilaya Nyasa kuwa ni moja kati ya Wilaya tajiri mkoani Ruvuma ikiwa na maeneo ya madini ya aina mbalimbali yakiwemo madini ya makaa ya mawe ambayo yanaweza kuingizia wilaya hiyo mapato makubwa kupitia kodi iwapo usimamizi utakuwa wenye tija.
Amesema wilaya ya Nyasa kuanzia mwanzo wa wilaya hadi mwisho ina miamba ambayo ikiwekezwa inaweza kuongeza mapato makubwa katika Halmashauri hiyo.
“Wilaya ya Nyasa ndani ya ziwa Nyasa kuna Samaki wa aina mbalimbali zikiwemo aina 400 za Samaki wa mapambo,wanaovua Samaki hao wananufaika kwa sababu wanauzwa nje kwa Dola,hakikisheni Halmashauri inasimamia mauzo ya Samaki hao ili kuongeza mapato’’,alisisitiza Kanali Thomas.
Katika kuhakikisha mapato yanaongezeka kupitia sekta ya utalii Mkuu wa Mkoa amesema ziwa hilo limebarikiwa kuwa na fukwe zinazofaa kuwekeza ambazo zinavutia kuanzia Chiwindi mpakani na nchi ya Msumbiji hadi Lituhi mpakani na wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
Kanali Laban pia ameagiza zoezi la usajiri wa wakulima liendelee ambapo hadi sasa ni wakulima 5000 tu wamesajiriwa katika wilaya ya Nyasa kati ya 16,000.
Ameagiza kilimo cha Pamoja kipewe kipaumbele ambacho kinawawezesha wakulima wengi kulima zao la aina moja katika sehemu moja.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amewaagiza ,madiwani katika Halmashauri hiyo kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo ukiwemo mradi wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 4.7 unatekelezwa katika vijiji vya Lituhi na Liuli.
RC Thomas amewaasa watumishi wa umma kuhakikisha wanajenga mahusiano mazuri ili utendaji wao uwe na tija pia amewataka kuacha kujiingiza kwenye madeni mengi yasiyokuwa na tija hali ambayo inashusha ari ya kufanyakazi.
Kuhusu changamoto zinazowakabili wazee zikiwemo za matibabu,ameagiza matibabu ya wazee yatolewe kwa wakati Pamoja na kuendelea kutoa vitambulisho vya matibabu bure kwa wazee,ingawa alitahadharisha kuwa Bima za afya zinazotolewa hazitoshelezi matibabu ya magonjwa yote.
Awali akizungumza kwenye kikao hicho,Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mheshimiwa Aziza Mangasongo alisema hadi sasa wazee waliotambuliwa kwenye wilaya hiyo ni 7528 kati yao waliopewa kadi za afya ni 4020.
Naye Mwenyekiti wa Wazee wa Wilaya ya Nyasa Yustine Mande akizungumza kwenye kikao hicho,amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kusikiliza kero za wazee na kuahidi kuzishughulikia.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma anaendelea na ziara ya kujitambulisha katika Halmashauri zote nane kwa kuzungumza na wazee,watumishi na waheshimiwa madiwani.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma
Septemba 22,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.