Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema walimu makada ni nguzo ya maarifa, maadili na uzalendo ndani ya Chama Cha Mapinduzi na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya itikadi kwa walimu makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Ruvuma yaliyofanyika kwa siku mbili katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania tawi la Songea kilichopo Manispaa ya Songea.
“Kupitia nyinyi walimu makada tunaunda msingi wa taifa lenye maadili, maarifa na lenye mwelekeo, katika zama hizi za mabadiliko ya kisera na uchumi, mnapaswa kuwa mstari wa mbele kusimamia na kusambaza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita, tumeshuhudia maboresho makubwa katika sekta ya elimu, afya, miundombinu na teknolojia,” alisema Kanali Ahmed.
Amewataka walimu hao kutambua kuwa wao ndio mabalozi wa chama katika sekta ya elimu kwa kuwa ndio waandaaji wa kizazi kijacho cha viongozi wa taifa hivyo wanapaswa kufundisha kwa mfano na si maneno.
Kanali Ahmed amewasisitiza walimu hao kusimamia haki, kutenda kazi kwa uadilifu, kuweka mbele maslahi ya watu, kuwa watetezi wa maadili katika jamii na wachambuzi wa sera za maendeleo na kutokuwa watazamaji wa mafanikio ya chama badala yake wawe washiriki katika mafanikio hayo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.