MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amekagua miradi ya ujenzi wa majengo ya hospitali mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma katika Kata ya Mwengemshindo Manispaa ya Songea.
Akitoa taarifa ya mradi huo,Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa,Songea Dr.Magafu Majura ameyataja majengo yanayotekelezwa kwenye mradi huo kuwa ni jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la huduma za mionzi na jengo la huduma za kuchuja damu(Dialysis unit).
Amesema kuwa serikali imetenga shilingi bilioni nne kujenga jengo la OPD lenye ghorofa moja ambapo hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 75 na kwamba mradi unatarajia kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Akizungumzia mradi wa jengo la mionzi,Dr. Majura amelitaja jengo la kutolea huduma za kichunguzi ya mionzi ambalo ndani yake kuna mashine mbili za CT Scan na Digital X ray ambazo zinazofanya kazi,limekamilika kwa asilimia 100 na limeanza kutoa huduma za CT Scan.
Dr.Majura ameutaja mradi wa huduma za kiuchunguzi za Radiolojia kuwa una thamani ya Zaidi ya shilingi bilioni mbili ambapo utekelezaji wa mradi huo ulianza Machi 2023 na huduma za CT Scan zilianza kutolewa Aprili 2023.
“Huduma ya CT Scan imepunguza adha kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma ambao walikuwa wanapata huduma hii katika hospitali ya Kanda ya Mbeya na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili’’,alisema Dr.Majura.
Mradi mwingine ambao unatekelezwa ni ujenzi wa jengo la kisasa la kusafishia damu ambapo Dr.Majura amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Januari 2024 na unatarajia kukamilika Julai 2024 na kwamba jengo linagharimu shilingi milioni 600.
Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amepongeza serikali kutekeleza miradi hiyo inayokwenda sanjari na ununuzi vifaa vya kisasa katika hospitali hiyo ambapo ametoa rai kwa wananchi kutumia huduma za kisasa zinazotolewa katika hospitali hiyo.
Amesisitiza kuwa wananchi wanachohitaji ni upatikanaji wa huduma na sio muonekano wa majengo ambapo amewataka watumishi kutunza majengo na vifaa.
“Dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya afya karibu na tayari amefanya kwa kiwango kikubwa,utekelezaji wa Ilani umefanyika ,watendaji tuhakikishe majengo yote yanakamilika kwa asilimia 100’’,alisisitiza.
Ametoa rai kwa watumishi wote wa afya kutoa huduma kwa lugha rafiki kwa wagonjwa ambapo amesema kauli nzuri kwa wagonjwa zinampa matumaini ya kupona kabla ya kupata huduma.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa hospitali 28 za Rufaa za mikoa ambapo historia yake inaanzia mwaka 1920,mwaka 1961 ilikuwa hospitali ya Wilaya,mwaka1964 ilipandishwa hadhi na kuwa hospitali ya Mkoa,Songea na mwaka 2009 ilitangazwa kuwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.