Na Albano Midelo,Songea
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amekagua mradi wa maji katika Kijiji cha Lipaya Kata ya Mpitimbi wilayani Songea wenye thamani ya shilingi bilioni 1.9 na kuwaagiza RUWASA kuanza kuwaingizia ndani maji wananchi vijijini.
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa Mkuu wa Mkoa,Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Songea Mhandisi Mathias Charles amesema mradi huo umesanifiwa ili kuwahudumia wananchi 3,886 kutoka katika vijiji vitatu na kwamba chanzo cha mradi huo kina uwezo wa kuzalisha maji lita 3,196,800 kwa siku.
“Mkataba wa mradi huu ni miezi 12 kuanzia Mei 2022 hadi Mei 2023,kutokana na changamoto zilizojitokeza mradi haukukamilika hivyo umeongezewa hadi Januari 18,2024’’,alisema
Hata hivyo Mhandisi Charles amesema hadi sasa mradi umekamilika kwa asilimia 98 ambapo amezitaja kazi ambazo zimeshakamilika kwa asilimia 100 kuwa ni ujenzi wa vituo 17 vya kuchotea maji,ujenzi wa banio la maji,uzio, na ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita 100,000 ambalo limekamilika kwa asilimia 97.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewapongeza RUWASA kwa kuendelea kusimamia vema miradi ya maji hivyo kuunga mkono azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama maji kichwani.
Amesisitiza kuwa nia ya Rais Dkt. Samia ni kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama ambapo amewaasa wananchi kuwa tayari kulipa bili za maji ili miradi ya maji iwe endelevu.
“Ili wananchi waweze kulipa bili zao kikamlifu,nakuaagiza Meneja wa RUWASA hakikisha wananchi wanaingiziwa maji ndani ya nyumba zao hivyo kinachotakiwa ni kutoa elimu kwa wananchi’’,alisema.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amekemea tabia ya uharibifu kwenye vyanzo vya maji ambapo amewaagiza viongozi ngazi ya vijiji kuhakikisha wanashirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania TFS kulinda vyanzo vya maji na kuzuia shughuli zote za kibinadamu kwenye chanzo cha maji cha Matogoro B wilayani Songea kinachotegemewa na Manispaa ya Songea.
Naye Diwani wa Kata ya Mpitimbi Mheshimiwa Issa Kindamba amempongeza Rais Dkt.Samia kwa kutoa fedha nyingi za kutekeleza mradi huo ambao amesema unakwenda kupunguza umbali wa wananchi kutembea kufuata maji na kupunguza magonjwa yanayosambazwa na maji yasiyo salama.
Kukamilika kwa mradi huu kumeongeza upatikanaji wa maji safi na salama katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea kutoka asilimia 71.4 hadi kufikia asilimia 73.8
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.