Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ametembelea vituo vya mabasi vya Ruhuwiko na Mfaranyaki katika Manispaa ya Songea, kusikiliza kero, maoni, na mapendekezo ya wananchi pamoja na wafanyabiashara wa maeneo hayo.
Akiwa katika kituo cha mabasi cha Ruhuwiko, Kanali Ahmed amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau wote, hususan wananchi na wafanyabiashara, katika mipango ya ujenzi wa stendi na vibanda vya biashara ambapo ametoa maagizo kwa wilaya na wataalamu kuhakikisha kuwa maamuzi yanayofanywa yanazingatia ushirikiano wa pande zote.
"Ninaagiza ushirikishwaji mkubwa wa wadau wote mliopo hapa, kama kuna suala la kutaka kuhamisha au kukodishwa vibanda, kuboresha huduma za bodaboda na bajaji, ni lazima ushirikishwaji mkubwa uwepo baina ya Serikali, chama na wenye hizo bodaboda, ili mtakayoyaamua yaweze kutekelezeka kirahisi kwa sababu yatakuwa ni maamuzi yaliyotokana na sisi sote," alisema Kanali Ahmed.
Pia amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika maamuzi na kutekeleza kwa haraka makubaliano yanayofikiwa, ili kuboresha eneo husika kwa manufaa ya jamii yote.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Kapenjama Ndile, ameeleza kuwa kituo cha mabasi cha Ruhuwiko kina umuhimu mkubwa kutokana na shughuli nyingi za biashara zinazofanyika hapo, hivyo amesema kuwa Manispaa ya Songea ina mipango madhubuti ya kuboresha eneo hilo.
Katika hatua nyingine, Meneja wa TANROAD Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Saleh Juma, amezungumzia msongamano wa magari unaosababishwa na malori mengi yanayobeba makaa ya mawe, akieleza kuwa ujenzi wa barabara mpya ya mchepuko (Songea Bypass) utaanza hivi karibuni.
Amebainisha kuwa tayari wananchi waliopo pembezoni mwa barabara hiyo wameanza kulipwa fidia ili kupisha ujenzi, hivyo amewahakikishia wananchi kuwa changamoto hiyo inashughulikiwa.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Mhe. Michael Mbano, amekiri changamoto ya vumbi na tope katika kituo cha mabasi cha Ruhuwiko wakati wa mvua, na amesisitiza kuwa hatua madhubuti zinaendelea kuchukuliwa ili kuimarisha mazingira ya eneo hilo.
Ameongeza kuwa Ruhuwiko ni eneo linalokua kwa kasi, na ni lango muhimu kwa wageni wanaoingia na kutoka mkoani kutokana na uwepo wa uwanja wa ndege.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.