Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amewataka wadau wa elimu kuweka nguvu kwenye vipaumbele ambavyo vitamsaidia mwanafunzi kufanya vizuri kitaaluma ikiwemo usimamizi mzuri wa sekta ya elimu katika mkoa.
Ametoa rai hiyo wakati akizungumza katika mkutano wa wadau wa elimu Mkoa wa Ruvuma, uliofanyika katika ukumbi wa Chandamali mjini Songea.
Kanali Ahmed amesema wataalamu wa elimu wanazifahamu vizuri changamoto zote zinazojitokeza katika sekta ya elimu na kupelekea mkoa kufanya vibaya kitaaluma, hivyo amesisitiza usimamizi na ubunifu katika maeneo yao.
Ametoa maagizo kwa viongozi na watendaji kusimamia malengo ya ufaulu kuanzia ngazi ya kata hadi juu, kuwatambua walimu wanaofanya vizuri, shule kushiriki katika kilimo kwa lengo la kumfundisha mwanafunzi kujitegemea na kupunguza changamoto ya chakula shuleni, na wadau wote kushirikiana kuwahamasisha wazazi kuchangia chakula na watendaji wa elimu kata kusimamia uratibu mzuri wa chakula shuleni.
Naye Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Ruvuma, Mwalimu Frolence Ngua, amebainisha kuwa utoro wa rejareja kwa baadhi ya watahiniwa, baadhi ya walimu kutomaliza mada kwa wakati, baadhi ya wazazi kuwashawishi watoto wao kufanya vibaya kwenye mitihani ya kitaifa, na upungufu wa walimu kwa ujumla na baadhi ya masomo ni sababu zinazosababisha ufaulu kushuka kwenye halmashauri.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, amewataka wadau wa elimu kutambua kuwa suala la elimu ni tofauti na sekta nyingine.
Amewasisitiza wadau wa elimu kwamba Mkuu wa Mkoa na Afisa Elimu Mkoa wasibebeshwe mzigo mzito katika elimu, na wadau wote wanatakiwa kutambua uwepo na wajibu wao na mzigo huo utakuwa mwepesi kwao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.