Na Albano Midelo,Songea
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed ametahadharisha kuwa shughuli za kiuchumi zisipofanywa kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam zinaweza kuharibu mazingira na kutishia mustakabali wa Maisha ya viumbehai.
Kanali Abbas ametoa tahadhari hiyo wakati anazungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani ambazo kimkoa zimefanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea na kuhudhuriwa na wadau wa Habari na na wanahabari.
“Kuna uchimbaji wa madini unafanyika kwa mtazamo ni shughuli ya kiuchumi kama isipofanywa vizuri kwa kuzingatia sheria,kanuni na ushauri wa kitalaam,unaweza kugeuka uchumi wenye kuharibu mustakabari wa maisha ya watu’’,alisisitiza.
Amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema uandishi wa Habari na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi,inakwenda kuugusa muhimili wa Habari ili wanahabari wakafanye kazi ya kuhabarisha umma kuhusu madhara yanayoweza kutokea kwa kutozingatia kanuni na sheria za uendeshaji wa shughuli za kiuchumi hivyo kusababisha mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa.
Amesema Rais Dkt.Samia amefanya kazi kubwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo ameweza kuanzisha mikakati na program mbalimbali ili kuhakikisha taifa na Dunia inaendelea kuwa salama kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Amebainisha kuwa hivi karibuni Rais Samia amezindua mkakati wa nishati safi ikiwa ni sehemu ya uendelezaji wa kampeni za kupambana na mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa.
Amesema madhara yameanza kujitokeza ambapo hivi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la joto kwenye uso wa dunia,pia kumekuwa na uyeyushaji wa barafu kwenye bahari na kusababisha ongezeko la maji ambalo pia limesababisha madhara mengi ikiwemo elnino na lanina.
Ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kumetokea madhara mbalimbali kama vimbunga ambapo hivi karibuni kimetokea kimbunga Hidaya ambacho kimeleta madhara makubwa.
Amesema madhara ya mabadiliko ya tabianchi ni mengi na kwamba yasipoelezwa vizuri kwa wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari, wananchi wanaweza kuendelea kufanya shughuli za kiuchumi bila kufuata kanuni na sheria,hivyo amesisitiza kuyatunza mazingira ili Taifa liendelee kuwa salama.
Akizungumzia maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya Habari Duniani,Kanali Abbas amewapongeza wanahabari kwa kufanya kazi nzuri ya kuhabarisha umma kazi mbalimbali zinazofanyika na serikali ndani ya Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo ametahadharisha kuwa wakati wanahabari wanatekeleza majukumu yao,wasiache kuangalia utekelezaji wa 4R za Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Ameahidi serikali ya Mkoa wa Ruvuma ipo tayari kushirikiana na wanahabari na kwamba yupo tayari kutoa kila aina ya ushirikiano unaohitajika ili kuhakikisha kazi ya wanahabari inakuwa nyepesi na matakwa ya muhimili wa kuhabarisha umma haukwami.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Kapenjama Ndile amesema katika Tanzania sheria zinawapa heshima kubwa waandishi wa Habari na kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoheshimu uhuru wa Habari.
Ndile amesisitiza kuwa huwezi kuheshimu vyombo vya Habari bila kuheshimu wanahabari wenyewe ambapo amesema wanahabari wamefanyakazi kubwa iliyotuka katika wilaya ya Songea na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Ruvuma Amon Mtega amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuyaunganisha makundi mbalimbali wakiwemo wanahabari .
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.