Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ameipongeza kampuni ya MANTRA TANZANIA ROSATOM kwa kuwekeza katika mradi wa kimkakati wa madini ya Uranium ambayo yanapatikana Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma.
Pongezi hizo amezitoa baada ya kutembelea mradi huo na kujionea maendeleo yake ambapo amesema mradi huo ni mkubwa kwa kuwa ukianza kazi Tanzania itakuwa ni moja kati ya nchi 10 za wazalishaji wa madini ya Uranium Duniani.
"Tumepata maelezo ya kutosha ya mradi huu na changamoto zake, tumepata fursa ya kutembelea kiwanda cha uzalishaji pia kuona mgodi wenyewe ulivyo, nichukue nafasi hii kuipongeza MANTRA Tanzania kwa Uthubutu wa kuja kuwekeza kwenye mradi wa kimkakati wa madini ya Uranium hapa nchini," alisema Kanali Ahmed.
Naye Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Alphonse Bikulamchi, amesema mradi huo umeanza tangu mwaka 2007 katika hatua za utafiti ambapo ulipatiwa leseni ya utafutaji madini, mwaka 2012 ulipatiwa leseni kubwa ya uchimbaji madini, na hadi kufikia sasa mradi unaendelea na maandalizi na ujenzi wa mradi wa majaribio.
Amezitaja faida zitakazopatikana baada ya mradi huo kukamilika kuwa utaenda kuinyanyua Tanzania na kuwa kati ya nchi 10 bora za uzalishaji wa madini ya Uranium, utaleta tija kubwa kwa Taifa na Mkoa wa Ruvuma, utaongeza ajira kwa watanzania, makusanyo ya Serikali kuongezeka na fedha za kigeni zitaweza kuingia.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.