Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amewataka wasimamizi wa elimu ngazi ya mkoa, wilaya na halmashauri kuhakikisha watoto wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa na waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanaripoti shuleni.
Ameyasema hayo wakati akifanya mkutano na waandishi wa habari kuhusu mwaka mpya wa masomo, uliofanyika katika ofisi yake iliyopo mjini Songea mkoani Ruvuma.
"Tuendeleze kasi na nguvu ya kusimamia zoezi hili ili liwe na mafanikio makubwa, kila mtoto anayestahili kandikishwa awe ameandikishwa, wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wahakikishe wote wanaripoti shule, viongozi waliopo katika mamlaka ya ngazi za wilaya na halmashauri wahakikishe wanaendelea kusimamia zoezi hilo ili wale ambao wanakiuka sheria wachukuliwe hatua,"alisema Kanali Ahmed.
Ameongeza kuwa zoezi hilo liende sawa na kuhakikisha wazazi wanawapatia watoto wao mahitaji stahiki ikiwemo sare za shule, shajara na kuhakikisha mtoto anapata chakula shuleni ili kumpunguzia vikwazo katika masomo yake.
Amemsisitiza kila mdau anayehusika na ujenzi wa miundombinu ya shule kuhakikisha anatimiza wajibu wake, miradi ya ujenzi inayojegwa izingatie ufanisi pamoja na kukamilishwa mapema ili wanafunzi waweze kuitumia miundombinu hiyo.
Kwa upande mwingine ameiagiza Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa na Halmashauri kuchukua hatua za kinidhamu kwa mtu yoyote anayerudisha nyuma usimamizi wa elimu katika mkoa, hivyo kusiwe na vikwazo vyovyote vya kumpokea wanafunzi shuleni kwa kisingizio chochote cha mzazi kutotimiza mahitaji ya shule kwa sababu ni muhimu kila mwanafunzi kuanza masomo na wenzake kwa wakati.
Pia, ametoa maelekezo kwa walimu wote kuhakikisha wanahudhuria darasani na kufundisha wanafunzi kama taratibu za kazi yao inavyowataka, malezi kwa kipindi chote wanafunzi wanapokuwa shuleni, kusimamia upandaji wa miti ya matunda kwaajili ya kujenga na kulinda afya za wanafunzi na kuhakikisha kila shule inakuwa na bustani za mbogamboga na shamba la mazao ya chakula lisilopungua hekari tatu.
Katika hatua nyingine, ametembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea (Songea Girls) na Sekondari ya Mfaranyaki kujionea hali ilivyo, ambapo amewasisitiza wazazi kuhakikisha wanajitolea kwa hali na mali ili kufanikisha suala la elimu, maafisa elimu kata kuwa wasimamizi wa awali, wasimamizi wa elimu ngazi ya msingi na sekondari pamoja na wadhibiti ubora kuhakikisha wanakuwa karibu na shule ili ubora wa elimu unaokusudiwa upatikane.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.