Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amewataka maafisa elimu kata wa Mkoa wa Ruvuma kujipanga upya na kutimiza wajibu wao ili kuondokana na changamoto za kutofanya vizuri kitaaluma.
Ametoa rai hiyo wakati akihitimisha mkutano wa tathmini wa maafisa elimu kata Mkoa wa Ruvuma, uliofanyika katika ukumbi wa kanisa la Anglican manispaa ya Songea.
Amewasisitiza kuwa wabunifu kutatua matatizo badala ya kulalamika, kuwasimamia walimu wafanye kazi na kutoa taarifa iwapo hawafanyi kazi ipasavyo, kuongeza kasi ya kusimamia wanafunzi kumudu stadi za KK kabla ya darasa la tatu, kuhakikisha mada zinakamilika na kupata muda wa marudio, na kuhakikisha kata zao zinafaulisha kwa asilimia zisizopungua 50 kwa daraja la kwanza hadi la tatu kwa mitihani ya kidato cha nne.
Kanali Ahmed amesema katika mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi kwa mwaka 2024 mkoa wa Ruvuma umefaulisha kwa asilimia 69.34 ambapo ufaulu umepanda kwa asilimia 0.28 kutoka ufaulu wa asilimia 69.06 kwa mwaka 2023, kwa darasa la nne ufauli ni asilimia 77 ukipanda kwa asilimia 1.76 kutoka ufaulu wa asilimia 76.01
Hata hivyo amesema kwa upande wa kidato cha pili na cha nne mwaka 2024 bado ufaulu sio mzuri, amesema ufaulu wa kidato cha pili ni asilimia 82.34 ambapo asilimia 17.66 ya wanafunzi wamebaki kidato cha pili ambao wengi huacha shule na kutofikia ndoto zao, ufaulu wa kidato cha nne ni asilimia 92.39 huku wenye daraja la kwanza hadi la tatu hawakufikia asilimia 50
Afisa Elimu Mkoa wa Ruvuma, Mwalimu Edith Mpinzile, amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu.
Ameeleza kuwa, serikali inaboresha miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji, kutoa fedha za uendeshaji wa shule, kulipa malimbikizo ya madeni, na kupandisha vyeo vya walimu, huku ikiendelea kusikiliza na kutatua kero za walimu na kuboresha hadhi ya walimu ili kuhakikisha Elimu inatoa matokeo bora.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.