Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amewahimiza wanawake wa mkoa wa Ruvuma kujitokeza na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025.
Ametoa wito huo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Songea kuelekea kilele cha siku ya wanawake duniani machi 8 mwaka huu ambayo kimkoa itafanyika uwanja wa Majimaji Manispaa ya Songea.
Kanali Ahmed amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo mwaka huu ni kuimarisha jamii kukuza usawa, haki na uwezeshaji wa wanawake, wasichana na wanaume kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Ameongeza kuwa maadhimisho hayo hujenga hamasa na ushiriki wa jamii katika kuchangia na kuleta usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, kutathmini utekelezaji wa agenda ya usawa wa kijinsia, haki na uwezeshaji wa wanawake katika masuala ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni nchini.
Amebainisha kuwa hadi sasa katika Mkoa wa Ruvuma wanawake 434 sawa na asilimia 22 wapo katika nafasi mbalimbali za maamuzi au uongozi hivyo wanawake wa mkoa wa Ruvuma wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu.
Katika hatua nyingine, Kanali Ahmed, amewasisitiza viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada kufikisha ujumbe kuhusu umuhimu wa malezi ya watoto ili kujenga familia na taifa imara.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.