Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amezindua mradi wa uanzishwaji wa dawati la ustawi wa jamii katika stendi kuu ya mabasi ya Manispaa ya Songea iliyopo Shule ya Tanga ambapo uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Kanali Ahmed, amesema mkoa wa Ruvuma unakabiliwa na changamoto ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, hasa Manispaa ya Songea, hali inayosababisha kujifunza na kujiingiza katika tabia hatarishi na hata kutumwa na watu wazima kwenye matukio ya wizi, uporaji, biashara za ngono, ulevi na matumizi ya dawa za kulevya.
"Katika Manispaa ya Songea kuna ongezeko la watoto wanaotumiwa katika uuzaji wa bidhaa kama vifungashio katika maeneo ya masoko, kuuza karanga, mayai na korosho, hali hii hufanya watoto wengi kuwa katika hatari ya kufanyiwa ukatili na kuhatarisha ustawi wao," alisema Kanali Ahmed.
Ameongeza kuwa uanzishwaji wa dawati la ustawi wa jamii katika stendi kuu utasaidia kuwabaini mapema watoto wanaposhuka kwenye magari, kuzuia kuingia mitaani, kubaini mahitaji na changamoto zao, na kuwapatia huduma muhimu na sehemu salama na kuwaunganisha tena na familia zao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Ruvuma, Victory Nyenza, amesema kwa kushirikiana na wadau wao ambao ni Railway Children Africa wanatambulisha mradi huo ambao utatekelezwa katika stendi kuu ya mabasi ya Manispaa ya Songea ukiwa na lengo la kuwasaidia watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.
Amesema lengo kuu ni kuwabaini watoto wanaoingia kupitia vituo vya usafirishaji ili kutathimini mahitaji yao na kuwapa huduma za kibinadamu za msingi za awali huku taratibu za usimamizi wa mashauri yao na kuwaunganisha na familia au ndugu zao ukiendelea.
Kw upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Hilda Ndambalilo, amesema mradi huo utaweza kuimarisha usalama wa mtoto hususani ambao wako mitaani wakifanyishwa kazi na kujumuisha wadau mbalimbali ambao watasaidia kuwaongoza watoto hao na kuhakikisha usalama wao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.