MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya Lilambo na Mletele ili vianze kuwahudumia wananchi.
Kanali Thomas ametoa maagizo hayo baada ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo.
Amesema kumekuwa na changamoto ya umaliziaji wa miradi hivyo ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Songea kutoa fedha za kumalizia vituo vya afya.
Amesema serikali inaendelea kutoa mabilioni ya fedha kutekeleza miradi mbalimbali ambapo Serikali kupitia mapato ya ndani katika Manispaa ya Songea imetoa shilingi milioni 514 kutekeleza ujenzi Kituo cha Afya Lilambo na zaidi ya shilingi milioni 545 zimetolewa na serikali Kuu kupitia Global Fund kutekeleza ujenzi kituo cha afya Mletele.
“Nichukue fursa hii kuwapongeza Manispaa ya Songea kwa kusimamia ujenzi wa kituo cha Afya Lilambo ambacho kinatumia mapato ya ndani ,hata hivyo ongezeni kasi ili mkamilishe ujenzi wa Kituo hiki ulioanza mwaka jana “,alisisitiza RC Thomas.
Mkuu wa Mkoa pia amekagua ujenzi wa madarasa 14 kati ya 76 yanayojengwa katika shule za sekondari Manispaa ya Songea kwa gharama ya shilingi bilioni 1.5.
Ameagiza ujenzi wa madarasa hayo na samani zake kukamilika kama ilivyopangwa kwa kuzingatia viwango ili yaanze kutumika Januari 2023.
Amewaagiza wakuu wa Wilaya kujenga utamaduni wa kukagua mara kwa mara miradi yote ya maendeleo ambayo serikali inatoa fedha.
Akitoa taarifa ya miradi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa,Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt.Federick Sagamiko amesema katika kipindi cha Julai 2021 hadi Oktoba 2022,Manispaa hiyo imepokea shilingi bilioni 2.7 toka serikalini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za elimu,afya,Utawala na Maendeleo ya Jamii.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Pololet Mgema amesema licha ya changamoto zilizopo ujenzi wa madarasa 96 katika Wilaya hiyo unaendelea vizuri na wanatarajia kumkabidhi madarasa hayo Mkuu wa Mkoa Desemba 10 mwaka huu.
Amewaagiza waandisi wanaosimamia miradi kuwa kwenye miradi wakati wote ili itekelezwe kwa viwango.Ameahidi dosari zote zilizojitongeza kwenye ukaguzi kufanyiwa kazi haraka.
Wilaya ya Songea inaundwa na Halmashauri tatu za Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Halmashauri ya Madaba na Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Novemba 28,2022.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.