MKUU wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas,amewataka wananchi wa mkoa huo kuhakikisha wanashiriki vyema zoezi la sensa ya watu na makazi ili kuisaidia serikali kupata takwimu sahihi pale inapotaka kupanga mipango ya maendeleo kwa wananchi wake.
Kanali Thomas ametoa wito huo jana wakati akizungumza na wananchi na viongozi wa wilaya Namtumbo,akiwa katika ziara ya kuhamasisha wananchi kujiandaa kushiriki zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika tarehe 23 wiki ijayo.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa na kuhakikisha watu wenye ulemavu,watoto na wanawake wanakuwa mstari wa mbele na kujitokeza kuhesabiwa na kamwe wasijaribu kuwaficha majumbani kwa kuwa ni kosa na hawatawatendea haki.
Katika hatua nyingine mkuu wa mkoa,amewakumbusha wananchi juu ya suala la kujiwekea akiba ya chakula kama tahadhari ya kutokea na kupatwa na tatizo la njaa katika familia zao.
Alisema hali ya uzalishaji katika msimu wa kilimo 2021/2022 haukuwa mkubwa,kutokana na changamoto ya upatikanaji wa pembejeo kwa baadhi ya wakulima,hata hivyo kiasi cha chakula kilichozalishwa ni lazima kitunzwe.
Alisema,kufuatia wimbi kubwa la wafanyabiashara kutoka mikoa mingine na nchi jirani walioingia kwa wingi kwa ajili ya kununua mahindi ni dhahiri kuwa chakula kilichozalishwa msimu 2021/2022 hakitatosheleza,hivyo ni muhimu wananchi kuchukua tahadhari hiyo badala ya kuuza chakula chote kutokana na tamaa ya fedha.
Aidha Kanali Laban, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuondoa ruzuku kwenye pembejeo ambapo bei ya mbolea katika msimu wa kilimo 2022/2023 itashuka kutoka Shilingi 120,000 hadi shilingi 70,000 kwa mfuko mmoja.
Alisema, hayo ni mafanikio makubwa kwa serikali hasa ikizingatiwa kuwa,wananchi wa mkoa wa Ruvuma wanategemea shughuli za kilimo kwa ajili ya kuendesha maisha yao ya kila siku.
Kanali Laban,amewaonya watendaji wa serikali watakaosimamia ugawaji wa pembejeo hizo kuepuka upendeleo na kutojihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa zoezi la ujazaji wa fomu kwa ajili ya kuwatambua wakulima.
Naye Waziri wa nchi ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Jenista Mhagama amewaomba Watanzania kuendelea kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kutekeleza majukumu yake vizuri.
Alisema,licha ya matatizo vita kati ya Ukraine na Urusi iliyosababisha kupanda kwa baadhi ya bidhaa na gharama ya maisha,lakini Rais Samia anafanya kazi kubwa ya kutatua changamoto mbalimbali kwa wananchi ikiwamo kuendelea kutoa fedha kwa kaya maskini na kuondoa ruzuku kwenye mbolea.
Mhagama,amewaomba wakulima kutumia muda wao kwenye shughuli za kilimo ili kuongeza uzalishaji wa chakula mashambani kwa kuwa, mazao ya chakula hususani zao la mahindi limekuwa zao kubwa la biashara.
Diwani wa kata ya Luchili Othman Njovu alisema,wananchi wa kata hiyo wataendelea kushirikiana na serikali katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwamo zoezi la sensa ya watu na makazi.
Njovu amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zao katika kuwatumikia wananchi na kuondoa ruzuku kwenye pembejeo za kilimo ambapo alieleza kuwa,hatua hiyo itaongeza uzalishaji wa mazao katika msimu wa kilimo 2022/2023.
“wananchi wa kata ya Luchili wamejiandaa na wako tayari kwa ajili ya kuhesabiwa siku ya tarehe 23 mwezi huu,hatutaki kuiangusha serikali yetu kwenye mambo muhimu ya maendeleo”alisema Njovu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.