MKUU wa kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Ruvuma Salum Morimori,amewataka madereva kutii, kuzingatia sheria na alama za usalama Barabarani kama zinavyoelekeza ili kuepuka ajali ambazo hupelekea watu kupoteza maisha au kuwasababishia ulemavu wa kudumu.
Morimori ametoa kauli hiyo jana, alipokuwa akizungumza na madereva wa mabasi yaendayo mikoani baada ya kufanya ukaguzi wa kustukiza katika kituo kikuu cha mabasi mjini Tunduru.
Alisema, baadhi ya madereva wa mabasi hawataki kuzingatia sheria na kufuata alama za barabarani na kutoa onyo kwa madereva wazembe kuwa, Jeshi la Polisi litawachukulia hatua kali ikiwamo kuwafikisha mahakamani wale wote wasiotaka kuzingatia au kufuata sheria zilizopo.
Alisema,kumekuwa na tabia ya madereva wa vyombo vya moto hasa mabasi ya abiria kuvunje sheria za usalama barabarani kwa makusudi na kusababisha ajali huku wakiwa wanazitambua sheria hizo.
“unakuta dereva anajua kabisa kwamba anavunja sheria za usalama barabarani lakini anaendelea kwa makusudi, tabia hii inachangia sana kuongezeka kwa ajali,natoa rai kwa madereva na wananchi wa mkoa wa Ruvuma kuhakikisha wanafuata na kuzingatia sheria hizo za barabarani”alisema Afande Morimori.
Kwa mujibu wa Morimori,kumekuwa na matumizi na tabia mbaya ya alama kama vile kupita kwa mwendo kasi zaidi ya spidi hamsini(50)kwenye makazi ya watu na kwenye vivuko(Zebra).
“kuna madereva wanaovuta bangi na kunywa pombe,watu kama hao tutawashughulikia kwa kuwawka maabusu na kuwafikisha mahakamani,Ruvuma hatutaki madereva wazembe huu ni mkoa salama”alisema.
Alisema,wakati mwingine madereva kuongea na simu bila kujali usalama wa watumiaji wengine wa barabara hizo, na kuwaomba wananchi wakiona dereva anaongea na simu au kuendesha gari kwa mwendo kasi ni vyema kutoa taarifa kwa Askari wa usalama barabarani.
Alisema, sio vizuri na wala haikubariki kisheria kwa abiria kuwa sehemu ya tatizo kwa kufurahia mwendo kasi wa dereva ambao unaweza kuhatarisha maisha yao, badala yake kulisaidia Jeshi hilo kuwafichua madereva wasiotaka kuzingatia sheria hizo.
Amewaomba wananchi wa mkoa wa Ruvuma,kuendelea kuzingatia na kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali ambazo zimekuwa chanzo cha kupoteza maisha ya watu wengi na nguvu kazi ya Taifa.
Katika ukaguzi huo ulioongozwa na Mkuu huyo wa kikosi cha usalama mkoa kwa kushirikiana na askari wa usalama barabarani wilayani Tunduru, baadhi ya magari yalikutwa na makosa mbalimbali ikiwamo matairi kuwa na vipara na madereva kuendesha kwa mwendo kasi ambapo wale waliokutwa na makosa hayo waliandikiwa faini na kutakiwa kufanya marekebisho ya kasoro hizo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.