BIASHARA ya madini ya makaa ya mawe mkoani Ruvuma imeshamiri baada ya mauzo jumla ya makaa ya mawe ya tani 450,675.32 ndani ya nchi na tani 1,060,699.05 ziliuzwa nje ya nchi katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2022.
Uchimbaji na uuzaji wa makaa ya Mawe Mkoani Ruvuma ulianza mwaka 2011 kukiwa na Kampuni moja tu ambayo ni Tancoal Energy Ltd.
Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Hamis Kamando anasema,mwaka 2019 wadau wengi walijitokeza na kufanya uwekezaji katika shughuli za Makaa ya Mawe hali iliyosababisha kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hayo kuanzia mwaka 2020.
Katika kipindi cha hivi karibuni, Makaa ya Mawe yamekuwa yakihitajika sana ulimwenguni kama chanzo cha nishati na hivyo kuwa moja ya chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali.
Hadi kufikia Juni 30,2022, Ofisi ya Madini Ruvuma ilikuwa imekusanya kiasi cha Shilingi zaidi ya Bilioni 21,sawa na asilimia 179 ya lengo la Mwaka huo.
Katika Mwaka huu wa fedha 2022/2023, Ofisi ya Madini Ruvuma ilipangiwa kukusanya zaidi ya Shilingi Bilioni 26 na kwamba hadi kufikia Juni 2023,Ofisi ya Madini Ruvuma ilifanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 34.
Madini ya makaa ya mawe huuzwa ndani ya nchi, nchi zinazotuzunguka,barani Ulaya na Asia kupitia bandari ya Mtwara na Dar es Salaam.
Katika Mkoa wa Ruvuma,kuna jumla ya wachimbaji 14 wanaochimba Makaa ya Mawe na kwamba katika Mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha Madini ya Makaa ya Mawe kilichouzwa ni jumla ya tani 639,482.55 ziliuzwa ndani ya nchi na tani 837,846.29 ziliuzwa nje ya nchi.
Faida za madini ya makaa ya mawe mkoani Ruvuma ni,Kuongezeka kwa mapato ya Serikali,Kuongeza kipato kwa mtu mmoja mmoja na kupunguza utegemezi kutokana na ajira zilizopo katika uchimbaji wa Makaa ya Mawe.
Faida nyingine ni kuongeza fedha za kigeni nchini kutokana na madini hayo kuuzwa nchi za nje na Kuongezeka kwa mapato ya Halmashauri yatokanayo na ushuru wa huduma unaotozwa kwenye madini yanayochimbwa.
Shughuli za utafiti na uchimbaji wa makaa ya mawe katika mkoa wa Ruvuma zinafanyika katika Wilaya ya Mbinga maeneo ya Mbalawala, Mbuyula, Paradiso,Ntunduwaro,Amanimakoro na Ngaka, katika Wilaya ya Songea katika maeneo ya Muhukuru, Mdunduwalo,Njuga na kikunja na Wilaya ya Nyasa maeneo ya Malini.
Waziri Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa mwaka 2023 ametembelea na kukagua mgodi wa makaa ya mawe wa Kampuni ya Jitegemee katika Kijiji cha Ntunduwaro wilayani Mbinga ambapo ameridhishwa kwa kushamiri kwa biashara hiyo.
Waziri Mkuu alifurahishwa na biashara ya makaa ya mawe baada ya kutembelea mgodi mmoja tu wa Jitegemee ambapo alielezwa mgodi umetoa ajira za kudumu 85,ajira za muda 150 ambapo alisema hiyo ni faida kubwa kwa wananchi na serikali ambayo inapata mapato makubwa kutokana na kodi na tozo mbalimbali.
Mkoa wa Ruvuma una hazina ya makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 227 ambayo yanatarajiwa kuchimbwa kwa miaka 300.
MKOA wa Ruvuma umeshika nafasi tatu katika kuchangia Pato la Taifa huku sekta ya Madini pekee hadi kufikia Juni 2023 imeingiza zaidi ya shilingi bilioni 34.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.