Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mheshimiwa Kisare Makori amewaongoza wanawake mkoani Ruvuma kuadhimisha siku ya wanawake duniani ambayo kimkoa imefanyika katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema maadhimisho hayo yanalenga kujenga hamasa na ushiriki katika kuleta usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.
Amebainisha kuwa moja ya sababu ya kaya kuendelea kuwa maskini ni wanawake kunyimwa haki ya kumiliki rasilimali ardhi, kukosa gharama za kuwawezesha kupata huduma za kifedha, haki ya kupata Elimu na ya kuchaguliwa kama kiongozi katika jamii ambapo Serikali ya awamu ya sita imesimamia haki na kujenga usawa katika jamii.
Amewasihi wanawake kutoa taarifa wanapokutana na matukio ya unyanyasaji au ukatili wa aina yoyote huku akiwataka kuendeleza ushirikiano katika kutoa Elimu na kupinga ukatili na unyanyasaji, kuwaelimisha na kuwapatia fursa stahiki watoto wa kike na kuwatengenezea mazingira bora ya kujifunza na kufundisha.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Makori mebainisha kuwa katika mkoa wa Ruvuma mwaka 2024/25 zaidi ya shilingi bilioni 4 zilitengwa kwa ajili ya kutoa mikopo ya asilimia 10 katika halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, na hadi kufikia sasa zaidi ya milioni 900 zimetolewa kwa vikundi 146 vya wanawake, hivyo wanawake wanapaswa kuanzisha vikundi na shughuli za ujasiliamali ambazo zitawainua kiuchumi na kuwawezesha kurudisha fedha wanazokopa.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia imefanya marekebisho ya Sheria mbalimbali na kutengenezea miongozo ambayo inawapatia wanawake fursa kubwa hivyo wanawake wanatakiwa kupambana ili kuhakikisha wanazipata fursa hizo.
Kwa upande wake Mratibu wa maadhimisho hayo Mkoa wa Ruvuma, Xsaveria Mlimira, amesema maadhimisho hayo yanawakumbusha kuielimisha jamii juu ya haki za binadamu hususani wanawake na watoto.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.