WANANCHI mkoani Ruvuma wamemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu kwa kutoa fedha ambazo zimewezesha kujengwa kwa sekondari mpya zenye mazingira ya kuvutia katika Halmashauri zote nane.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Grace Quietine amesema Rais ametoa shilingi milioni 470 kujenga sekondari mpya katika Kata ya Lusonga ambayo imekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.
Amesema kiasi hicho cha fedha kimewezesha kujenga jengo la utawala,vyumba nane vya madarasa,maabara tatu,jengo la TEHAMA,jengo la maktaba,vyoo matundu 20 na sehemu ya kunawia maji mikono wanafunzi.
Amesema tayari wanafunzi wa kidato cha kwanza wamesajiriwa na kuanza masomo ambapo hivi sasa shughuli za umaliziaji zinaendelea zikiwemo za kuweka mfumo wa gesi na maji katika majengo ya maktaba na kwamba Halmashauri pia imeongeza fedha za kukamilisha mradi huo ambapo hadi sasa zaidi ya shilingi milioni 492 zimetumika.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Chiza Marando amesema anamshukuru Rais kwa upendeleo wa pekee wa kuwapatia kiasi cha shilingi bilioni 1.4 kujenga sekondari mpya tatu za mfano katika wilaya hiyo ambazo zimekamilika na kuanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza.
Amesema kila sekondari imepewa shilingi milioni 470 na kuzitaja sekondari hizo kuwa zimejengwa katika kata za Nakayaya,Majimaji na Lukumbule na kwamba kila shule imejenga jengo la utawala,madarasa nane,vyoo,samani,maabara tatu,jengo la TEHAMA na maktaba.
“Shule zote tatu zinaendelea na hatua za ukamilishaji,lakini tumeshazisajiri na tumeshazifungua,wanafunzi wanaendelea kusoma, tunamshukuru sana Rais kwa kutumbuka Tunduru’’;alisema Marando.
Hata hivyo amesema kufunguliwa kwa shule hizo kumepunguza kero ya wanafunzi kwenye kata hizo kusafiri umbali mrefu kufuata sekondari.
Rais Samia pia ametoa shilingi milioni 470 kujenga sekondari mpya katika Kata ya Msisima Halmashauri ya Namtumbo na kwamba sekondari hiyo imefunguliwa na wanafunzi wameanza masomo.
Halmashauri nyingine ambazo zimepata fedha za ujenzi wa sekondari mpya ni Manispaa ya Songea katika Kata ya Mshangano zimetolewa shilingi milioni 470 kujenga sekondari ya Luhira.
Kata nyingine ni ya Amanimakoro Halmashauri ya Mbinga,Kata ya Riwundi wilaya ya Nyasa,Kata ya Lituta Halmashauri ya Madaba na Kata ya Kizuka Halmashauri ya wilaya ya Songea.
Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 7.7 kujenga sekondari mpya 11 katika Mkoa wa Ruvuma kupitia program ya kuboresha Elimu ya sekondari nchini (SEQIUP).
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Februari 9,2023.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.