Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeiandika upya historia ya maendeleo mkoani Ruvuma kwa kuwekeza zaidi ya shilingi trilioni 1.18, hatua inayogeuza maisha ya wananchi na kuufanya mkoa huo kuwa mfano wa kuigwa kitaifa katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Mary Makondo, amesema hayo wakati wa hafla ya utambulisho wa mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara ya lami ya kilomita 60 kutoka Likuyufusi (Manispaa ya Songea) hadi Mkayukayu (Halmashauri ya Wilaya ya Songea), ambapo serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 110 kutekeleza mradi huo kwa kipindi cha miezi 27.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, alibainisha kuwa maendeleo haya si ya bahati nasibu bali ni matokeo ya dhamira ya dhati ya Serikali ya Rais Samia kuweka ustawi wa mwananchi mbele.
Alisema Serikali imetumia shilingi bilioni 192.3 katika sekta ya elimu ambapo vyumba vya madarasa 1,717 vimejengwa, shule mpya 67 zimeanzishwa, mabweni 95, maabara 98, na nyumba za walimu 106 zimejengwa kwa viwango vya kisasa.
Alisema serikali imewekeza bilioni 45.3 kwenye sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya 16, hospitali za wilaya 5, zahanati 47, na kuimarisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma.
Aliongeza kuwa Vifaa tiba vya kisasa, magari ya wagonjwa 21, na magari maalum ya kusambaza chanjo vimeongeza upatikanaji wa huduma.
Makondo alisema Kwa kutumia shilingi bilioni 301.2, Serikali imejenga barabara ya lami Mbinga–Mbambabay (66 KM), barabara nyingine za lami zenye urefu wa 141.75 KM, na madaraja makubwa yenye urefu wa 231.5M.
Alisema Miundombinu hii imeunganisha wilaya, kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza kipato cha wakulima waliokuwa hawana soko la uhakika.
Kwa uwekezaji wa shilingi bilioni 168.7, vijiji vyote 554 vya Mkoa wa Ruvuma sasa vinaunganishwa na gridi ya taifa. Hali hii imefungua fursa za biashara ndogo, viwanda vidogo na ujasiriamali wa wanawake na vijana.
“Tunaangalia runinga na watoto wanasoma hadi saa nne usiku,” anasema Bi Frida Ligola wa Kijiji cha Lundo, Wilaya ya Nyasa.
Kulingana na Katibu Tawala huyo,Serikali imetumia bilioni 228.92 kuboresha huduma ya maji, ikiwa ni pamoja na mradi mkubwa wa maji wa bilioni 145 katika Manispaa ya Songea ambao unatarajiwa kumaliza tatizo la mgawo wa maji.
Kuhusu sekta ya usafiri,amesema Serikali imetumia shilingi bilioni 141 kuboresha usafiri kwa kukarabati Uwanja wa Ndege wa Songea, kujenga bandari za kisasa Ndumbi na Mbamba Bay, na vituo vya mabasi vya kisasa. .
Katika sekta ya kilimo, serikali imetumia bilioni 96.8 kujenga maghala 28, kusambaza tani 118,292 za mahindi na pembejeo.
Chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, maendeleo hayabahatishi tena; yanapangwa, yanatekelezwa, na yanaishi kwenye macho ya kila mwananchi wa Ruvuma.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.