SHIRIKA la Ndege la Tanzania ATCL limerejesha safari za usafiri wa anga mkoani Ruvuma baada ya kukamilika ukarabati kiwanja cha ndege cha Ruhuwiko mjini Songea.
Serikali ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 37 kukarabati kiwanja cha ndege Songea na kuwezesha ndege aina ya Bombardier Q400 kuanza tena safari zake za kuruka na kutua katika Kiwanja cha Ndege cha Songea kuanzia Februari 17 mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya kushuka katika safari ya kwanza ya Bombadier kwenye uwanja wa Songea,Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea mjini Dkt.Damas Ndumbaro amesema kuanzishwa kwa safari ya anga mkoani Ruvuma ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.
“Ibara ya 58 ya Ilani ya CCM imetamka kwamba uwanja wa ndege wa Songea utajengwa,Ilani imetamka kwamba zitanunuliwa ndege 11 mpya,pia Ilani imetamka kuwa ATCL itaongeza safari za ndege kutoka viwanja vinne mwaka 2015 hadi viwanja 13, mwaka 2021,Songea ni kiwanja cha 13,anasema Waziri Ndumbaro
Anasisitiza kuwa kiwanja cha Ndege Songea kitafungua anga la mkoa wa Ruvuma na kuruhusu wawekezaji na watalii kufika Ruvuma kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji na utalii hivyo kuchangia pato la taifa na kuinua uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Pololet Mgema anampongeza Rais kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 37 ambazo zimekamilisha ujenzi na ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Songea ambacho kimeanza kutumika rasmi kutua ndege kubwa.
Naye Meneja Kiwanja cha Ndege Songea Jordan Mchami anasema safari za ndege za ATCL zimerejeshwa mkoani Ruvuma kwa kuanzia safari toka Dar es salaam hadi Songea zitakuwa siku ya Jumatano na Jumapili.
“Ndege itakuwa inaondoka Dar es salaam saa 1:00 asubuhi,itafika Songea saa 2:25 asubuhi,itaondoka Songea 2:50 asubuhi itafika Dar es salaam saa 4:10 asubuhi, kwa kuanzia nauli ni shilingi 252,000, kwenda na kurudi ni 372,000 natoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma na mikoa jirani kutumia ndege hii’’,anasema Mchami.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Februari 18,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.