Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema Halmashauri zote nane zimefikia kiwango cha kuridhisha cha upatikanaji wa maji ambapo tayari miradi 23 ya maji iliyogharimu shilingi bilioni 25.9 imekamilika.
Kanali Abbas amesema hayo wakati anazungumza na wanahabari ofisini kwake mjini Songea,kuelekea katika maadhimisho ya wiki ya maji ngazi ya Mkoa wa Ruvuma ambayo yanaanza Machi 16 hadi 22 mwaka huu.
Amebainisha kuwa upatikanaji wa maji vijijini katika Halmashauri ya wilaya ya Songea umefikia asilimia 78.1,Madaba asilimia 79.4,Tunduru asilimia 70.2,Halmashauri ya Mbinga asilimia 71,Mbinga Mji asilimia 76,Namtumbo asilimia 71 na Nyasa asilimia 60.1.
Hata hivyo amesema licha ya miradi hiyo iliyokamilika,kuna miradi ya maji 30 inayoendelea kutekelezwa yenye thamani ya shilingi bilioni 58.5 na kwamba miradi hiyo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi 264,747 na kuongeza asilimia ya upatikanaji wa huduma ya maji toka asilimia 70.9 hadi 87.
“Ipo miradi 22 ya kipaumbele inayotekelezwa kwa thamani ya shilingi bilioni 8.6,pia serikali imetenga shilingi bilioni 18.9 za kutekeleza miradi 38 ambayo itahudumia vijiji 66’’,alisema Kanali Abbas.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Mkoa pia unatekeleza program ya visima 40 kwa wastani wa visima vitano kwa kila Jimbo ambapo tayari visima virefu 30 vimechimbwa katika majimbo ya Nyasa,Songea,Tunduru na Namtumbo.
Ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa miji 28 unaotekelezwa katika Manispaa ya Songea kwa gharama ya Zaidi ya shilingi bilioni 145,upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Ruvuma utafikia katika kiwango cha wananchi wote kupata huduma ya maji safi na salama.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Komredi Odo Mwisho akizungumza kwenye mkutano huo na wanahabari amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maji katika Mkoa wa Ruvuma.
Amesema kabla ya uongozi wa serikali ya Awamu ya Sita upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Ruvuma ulikuwa ni chini ya asilimia 50 kwa uongozi wa awamu ya kwanza hadi ya Tano ambapo katika Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan upatikanaji wa maji umepanda kwa kiwango kikubwa hadi kufikia Zaidi ya asilimia 78.
Amesema kuwa hali hiyo inaonesha kuwa Rais Samia amedhamiria kwa vitendo kumtua mama ndoo kichwani na kumaliza kabisa kero ya upatikanaji wa maji na salama kwa wananchi
Kaulimbiu ya maji wiki ya maji mwaka huu ni Uhifadhi uoto wa asili kwa uhakika wa maji
Pichani ni Mwenyekiti wa CCM Ruvuma Komred Oddo Mwisho akizungumza na wanahabari kuelekea maadhimisho ya wiki ya maji Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.