Na Gustaph Swai - Rs Ruvuma
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amebainisha kuwa Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya ya uzazi na Watoto Nchini kwa lengo la kupunguza na kumaliza tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika.
Ameyasema hayo alipoongoza Kikao cha makabidhiano na majadiliano ya mwendelezo wa mfumo wa usafirishaji wa dharura kwa akina mama wajawazito, waliojifungua na watoto wachanga(M-mama) kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
"Serikali ya awamu ya sita inayodhamira ya dhati ya kuboresha huduma za afya ya uzazi na Mtoto Nchini kwa lengo la kupunguza au kumaliza tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika"
Amesisitiza kutoa kipaumbele kwa Rufaa kwa wazazi na Watoto wachanga na halmashauri kusimamia Mfumo wa M-mama kwa kuhakikisha Magari ya Wagonjwa yapo tayari wakati wote na kuweka uratibu mzuri kwa madereva ngazi ya jamii.
Amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha Halmashauri zimetenga bajeti zitakazowezesha shughuli za Rufaa kwa Mfumo wa M-mama kwa kila mwaka wa fedha.
Amewaagiza kuhakikisha vituo vyote vinavvyotoa huduma za Afya vinatumia mfumo wa M-mama ili taarifa za wanaopewa rufaa zifahamike na kuhakikisha wote wanaohusika kuratibu Mfumo wa M-mama wanatekeleza wajibu yao kwa weledi.
Sanjari na hayo Kanali Ahmed amesisitiza kujitahidi kudhibiti na kuwa makini na upotoshaji wowote unaofanywa ili malengo ya Serikali yasihujumiwe.
Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Hilda Ndambalilo amesema hadi sasa mfumo wa M-mama umewezesha kusafirisha jumla ya wagonjwa 1,938 kati yao akinamama wajawazito 1,664 na Watoto wachanga 274.
Naye Mratibu wa Mfumo wa M-mama Nyanda za Juu Kusini kutoka Pathfinder Magdalena Mwaikambo ameeleza kuwa Mfumo wa M-mama umeweza kupunguza ucheleweshwaji wa usafirishaji wa rufaa za kina mama na watoto wachanga wenye uhitaji.
M-mama ni mfumo wa usafirishaji wa dharura wa akinamama wajawazito, waliojifungua ndani ya siku 42, na watoto wachanga ndani ya siku 28.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.