Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta ya Elimu, Maji na afya katika mkoa wa Ruvuma.
Ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea.
"Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo hasa katika sekta ya elmu, afya, maji, barabara, nishati, kilimo na miundombinu mingine ikiwemo bandari, ili malengo ya miradi hiyo yafikiwe ni muhimu sisi sote kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi," alisema Kanali Ahmed.
Amebainisha kuwa mkoa umeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa maduhuli na mapato ya ndani katika halmashauri ambapo kwa mwaka 2023/24 Mamlaka ya Mapato Mkoa imekusanya shilingi bilioni 20.33 sawa na asilimia 117 ya lengo la makusanyo ya bilioni 17.43.
Amesema kwa upande wa Halmashauri jumla ya shilingi bilioni 31.46 zimekusanywa ambayo ni sawa na asilimia 112.85 ya lengo la kukusanya bilioni 27.88 kwa mwaka, hivyo ameipongeza Mamlaka ya Mapato TRA Mkoa, viongozi na wataalam wote wa halmashauri wakiongozwa na wenyeviti wa halmashauri.
Ameongeza kuwa katika sekta ya kilimo Mkoa umeendelea kufanya vizuri Kwa msimu wa kilimo wa 2023/24 mkoa umezalisha tani milioni 1,955,763.76 za mazao ya chakula ukilinganisha na mahitaji halisi ya Mkoa ni tani 470,000 na kuwa na ziada ya tani milioni 1,485,763.76 ambazo huuzwa ndani na nje ya mkoa na kuwapatia wananchi kipato.
Kanali Ahmed ameeleza mkoa umeendelea kuimarika kiuchumi kutokana na kuimarika kwa miundombinu, shughuli za uzalishaji mali, biashara na uwekezaji katika shughuli za uchimbaji madini hasa makaa ya mawe, maboresho ya uwanja wa ndege wa Songea pamoja na biashara na mikoa na nchi jirani za Msumbuji na Malawi.
Amebainisha kuwa kutokana na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, pato la mkoa (GDP) limeongezeka kutoka shilingi trilioni 5.1 mwaka 2029 hadi kufikia trilioni 7.17 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 40.4, pato la mtu kwa mwaka 2019 ni milioni 3.15 hadi kufikia milioni 3.72 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 17.8.
Kwa upande wa umeme mkoa umewezesha vijiji 541 kati ya vijiji 551 kuungwanishwa umeme sawa na asilimia 98.18 ya vijiji vyote, vitongoji 272 na migodi midogo ya uchimbaji madini inaunganishwa na umeme ili kuchochea maendeleo ya viwanda, kilimo na biashara ambapo Mhe. Rais Dkt. Samia ametoa bilioni 291 zilizowezesha utekelezaji wa miradi hiyo.
Katika sekta ya Elimu amesema miundombinu ya kujifunzia na kufundisha imeboreshwa kwa sehemu kubwa, kwa mwaka 2023/24 wanafunzi 27, 281 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza bila kuwepo kikwazo cha ukosefu wa vyumba vya madarasa na wanafunzi 41,662 sawa na asilimia 82.12 wameandikishwa kujiunga na darasa la awali kati ya lengo la wanafunzi 46,707 sawa na asilimia 93.66.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.