Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) inaendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja mkoani Ruvuma.
Lengo kuu ni kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, hivyo kuchochea uchumi na kupunguza umaskini.
TANROADS Mkoa wa Ruvuma inasimamia mtandao wa barabara wa kilomita 2,166.62, zikiwemo barabara kuu na barabara za mkoa.
BAJETI NA UTEKELEZAJI WA MIRADI
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Salehe Juma Mkwama anasema Katika kutekeleza majukumu yake, TANROADS inasimamia miradi mikubwa ya maendeleo, miradi midogo ya maendeleo, pamoja na matengenezo ya barabara na madaraja.
Miradi hii inatekelezwa kwa bajeti inayosimamiwa kupitia Makao Makuu ya TANROADS kwa kushirikiana na serikali na wadau wa maendeleo.
MIRADI MIKUBWA YA MAENDELEO
UJENZI WA BARABARA YA MBINGA – MBAMBA BAY
Barabara hii ya kilomita 66 ilijengwa na kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) kwa gharama ya Tsh. 129.36 bilioni. Mradi huu ulizinduliwa tarehe 24 Septemba 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan.
UJENZI WA DARAJA LA RUHUHU
Daraja la Ruhuhu lililopo katika Mto Ruhuhu unaomwaga maji yake ziwa Nyasa\, lina urefu wa mita 98.01 linaunganisha Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma na Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe. Ujenzi wa daraja hilo ulikamilika tarehe 15 Oktoba 2021 kwa gharama ya Tsh. 8.976 bilioni.
UKARABATI WA UWANJA WA NDEGE SONGEA
Ukarabati wa uwanja huu ulianza Aprili 2019 na kukamilika Machi 2023 kwa gharama ya Tsh. 37.09 bilioni. Mradi huu ulikuwa kwenye kipindi cha uangalizi hadi Septemba 2024.
UJENZI WA BARABARA YA KITAI - LITUHI - NDUMBI
Mradi huu wa kilomita 95.3 unatekelezwa kwa awamu tatu kwa kiwango cha lami:
• Kitai – Amani Makoro (Km 5): Ulianza Juni 2019 na kukamilika Agosti 2020 kwa Tsh. 6.957 bilioni.
• Amani Makoro – Ruanda (Km 35): Ujenzi ulianza Juni 2022 kwa Tsh. 60.481 bilioni.
• Ruanda – Lituhi – Ndumbi (Km 50): Ujenzi unaendelea kwa Tsh. 95.76 bilioni na unatarajiwa kukamilika Juni 2026.
UJENZI WA BARABARA YA LIKUYUFUSI – MKENDA
Barabara hii ya kilomita 124 ipo kwenye hatua za mwisho za kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi. Fidia ya Tsh. 5.19 bilioni imeshatathminiwa na kusubiri malipo kutoka Wizara ya Fedha.
UJENZI WA BARABARA YA LUMECHA–LONDO-MALINYI – LUPIRO
Mradi wa ujenzi wa barabara hii ya kilomita 512 inaunganisha
mikoa ya Ruvuma na Morogoro.
Serikali imesaini mkataba na kampuni ya China Civil Engineering ConstructionCorporation Ltd (CCECC) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu
kwa sasa utatekelezwa kwa Mfumo wa Sanifu na jenga ('Design and Build') ambao ni ujenzi wa barabara ya Lumecha - Londo - Malinyi - Lupiro
UJENZI WA BARABARA YA SONGEA – LUTUKIRA NA MCHEPUKO WA SONGEA
Mradi huu wa kilomita 116 unafadhiliwa na Benki ya Dunia. Ujenzi unatarajiwa kuanza wakati wowote baada ya kukamilika kwa mchakato wa zabuni.
MIRADI YA MADARAJA
DARAJA LA MITOMONI
Daraja lenye urefu wa mita 47.7 linaunganisha Wilaya za Nyasa na Songea Vijijini.
Mradi huu utatekelezwa kwa miezi 15 kwa gharama ya Tsh. 9.29 bilioni kwa ufadhili wa Serikali na Benki ya Dunia.
DARAJA LA MKILI
Daraja hili linafanana na la Mitomoni na linajengwa kwa Tsh. 3.19 bilioni kwa muda wa miezi 15.
DARAJA LA MKENDA
Daraja hili linaunganisha Tanzania na Msumbiji kupitia Mto Ruvuma. Zabuni yake ilitangazwa lakini ilihitajika kutangazwa upya baada ya mzabuni mmoja tu kujitokeza.
USANIFU WA BARABARA NA MADARAJA
Mbali na miradi inayoendelea, TANROADS inaendelea na usanifu wa barabara na madaraja muhimu kama:
• Barabara ya Mbamba Bay – Lituhi (Km 112.4)
• Barabara ya Mtwarapachani – Nalasi – Tunduru (Km 300)
• Barabara ya Madaba – Mundindi – Liganga – Mkiu (Km 46)
MATENGENEZO YA BARABARA NA HIFADHI YA BARABARA
Katika kuhakikisha barabara zinapitika muda wote, TANROADS mkoa wa Ruvuma imetenga Tsh. 17.9 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya barabara za muda maalumu na sehemu korofi.
Aidha, jitihada za kuhifadhi hifadhi ya barabara zinaendelea kwa kuweka vigingi na kutoa notisi kwa wavamizi.
Juhudi za serikali kupitia TANROADS mkoa wa Ruvuma zinaendelea kuleta maendeleo kwa kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja.
Haya yote yanalenga kuinua uchumi wa wananchi kwa kurahisisha usafiri, kuunganisha mikoa na kuimarisha sekta ya uchukuzi nchini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.