SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)mkoa wa Ruvuma, imeanza ujenzi wa barabara la Amanimakoro-hadi Ruanda yenye urefu wa km 35 kwa kiwango cha lami ili kurahisisha shughuli za usafiri wa wananchi na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Akizungumza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi alisema, barabara hiyo inajengwa na kampuni ya China Railway Sevent Group(CRSG) gharama ya Sh.bilioni 60.4 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.
Alisema,barabara ya Amanimakoro-Ruanda ni ya kimkakati na muhimu sana kiuchumi kwa kuwa ndiyo inayounganisha wilaya ya Mbinga na Nyasa na inatumika kusafirisha makaa ya mawe kutoka kwenye migodi iliyopo kwenye vijiji vya wilaya ya Mbinga kwenda mikoa mingine hapa nchini na nchi jirani.
Alisema,barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Kitai-Ruanda hadi Lituhi kuelekea Mbambabay kupitia bandari ya Ndumbi,ambapo serikali iko katika maandalizi ya kujenga kipande kingine kutoka Ruanda hadi bandari ya Ndumbi chenye urefu wa km 50 kwa kiwango cha lami.
Alisema, kwa sasa kazi ya ujenzi inaendelea vizuri na mategemeo ya serikali kwamba itakamilika kwa mujibu wa mkataba ifikapo mwezi Disemba mwaka 2023.
Alisema,itakapokamilika itatoa fursa kwa wananchi kuitumia barabara hiyo katika shughuli zao za maendeleo na kuwaomba wale wote wanaopitiwa na ujenzi wa mradi huo kuhakikisha kila mmoja anakuwa mlinzi na kutoa ushirikiano kwa mkandarasi.
Kwa mujibu wa Mlavi ni kuwa, kuwepo kwa mradi huo kwenye maeneo yao ni fursa kubwa kwani utawawezesha kufanya shughuli mbalimbali na kupata kazi ambazo zitawaingizia kipato.
Mlavi alisema wananchi hawana budi kutambua kwamba, barabara hiyo ni yao inajengwa kwa manufaa yao kwa hiyo wana wajibu wa kuitunza na kuhakikisha hakuna hujumu yoyote ikiwamo wizi wa vifaa vinavyoletwa kwa ajili ya mradi huo.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Amanimakoro na Ruanda wilayani Mbinga, wameipongeza serikali ya awamu ya sita kuanza ujenzi wa barabara hiyo ambayo inakwenda kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi katika wilaya za Mbinga na Nyasa na Taifa kwa ujumla.
Halfani Omari mkazi wa kijiji cha Amanimakoro alisema,barabara hiyo itakapokamilika itasaidia kufanya shughuli zao za kiuchumi na kurahisisha usafiri kati ya kijiji hicho na maeneo mengine ya wilaya ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma.
Aliongeza kuwa, kwa muda mrefu changamoto kubwa katika barabara hiyo ni vumbi la makaa ya mawe kuingia ndani ya nyumba zao pindi malori yanapopita, hivyo kusababisha madhara mbalimbali kama kukohoa na mafua ya mara kwa mara.
Frolian Kayombo mkazi wa kijiji cha Ruanda alisema,kutokana na ubovu wa barabara hiyo, kumesababisha kupanda kwa gharama za maisha,kukosekana kwa usafiri wa uhakika na hata bei bidhaa mbalimbali kuwa kubwa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.