Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma umeanza ujenzi wa awamu ya pili wa barabara ya Amanimakolo-Ruanda hadi Bandari ya Ndumbi yenye urefu wa kilometa 95 kwa kiwango cha lami.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma,Mhandisi Saleh Juma, amesema ujenzi huo utafanyika kwa awamu tatu, ambapo awamu ya kwanza iliyohusisha kilometa tano kutoka Kitai hadi Amanimakolo tayari imekamilika na barabara hiyo imeanza kutumika.
Kwa sasa, ujenzi wa awamu ya pili unaendelea kutoka Amanimakolo hadi kijiji cha Ruanda, umbali wa kilometa 35. Meneja huyo amebainisha kuwa kazi imeanza kwa kuweka tabaka la lami kwenye kipande cha kilometa mbili kati ya 35.
Aidha, ujenzi huu ni sehemu ya mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo awamu ya tatu itahusisha kipande cha Ruanda hadi Bandari ya Ndumbi wilayani Nyasa.
Saleh ameongeza kuwa ujenzi wa Bandari ya Ndumbi ulikamilika miaka miwili iliyopita na kinachosubiriwa ni ukamilishaji wa barabara ili bandari hiyo ianze kutumika kusafirisha bidhaa kutoka Ruvuma kwenda mikoa mingine na nchi jirani ya Malawi.
Alisisitiza kuwa TANROADS inaendelea kutekeleza mradi huu bila vikwazo, huku Serikali ikiendelea kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo ili kuondoa kero ya vumbi linalosababishwa na magari yanayosafirisha makaa ya mawe.
Kwa upande wake, Mhandisi wa TANROADS Ruvuma, Anselem Chambila, amesema kati ya kilometa 35 zilizopo kwenye mpango wa awamu ya pili, kilometa tano tayari zimeanza kujengwa na mbili ziko katika hatua za mwisho kukamilika. Ameeleza kuwa mradi huu unatekelezwa vizuri na wanachosubiri ni fedha za kukamilisha kipande kilichobaki ili wananchi waweze kunufaika na barabara hiyo.
Naye Meneja Mradi wa Kampuni ya China Railway Seventh Group (CRSG), GE Guanghua, amesema hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 40. Wakati huo huo, baadhi ya wananchi wa kijiji cha Amanimakolo wameipongeza Serikali kwa kuendelea na ujenzi wa barabara hiyo, huku wakiitaka TANROADS kumsimamia kwa karibu mkandarasi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuondoa adha ya usafiri.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.