Waziri wa Afya na Mbunge wa Songea Vijijini, Mheshimiwa Jenista Mhagama, amebainisha hatua madhubuti zinazochukuliwa na serikali ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Mpox nchini.
Akizungumza katika kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Ruvuma kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea, Waziri Mhagama ameeleza kuwa serikali imeandaa kampeni maalum ya siku 54 za kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa Mpox na jinsi ya kujikinga.
Amefafanua kuwa Mpox ni ugonjwa unaoambukizwa kwa kugusana moja kwa moja na mgonjwa, kukumbatiana, kubusiana, au kutumia vifaa vilivyotumiwa na mtu mwenye ugonjwa huo.
Amewasisitiza wananchi kuchukua tahadhari kwa kuzingatia usafi wa mwili na mazingira, pamoja na kufuata maelekezo ya wataalam wa afya huku serikali ikiendelea kuimarisha huduma za afya kwa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba na kuboresha huduma kwenye hospitali na vituo vya afya kote nchini.
Waziri Mhagama amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuimarisha sekta ya afya, ikiwemo ujenzi wa vituo vipya vya afya na upatikanaji wa dawa muhimu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema ugonjwa wa Mpox ni hatari sana hivyo amewasisitiza wananchi kuchukua tahadhari kama wataalam wanavyoelekeza.
Mnamo mwezi Machi mwaka huu, tetesi za uwepo wa wagonjwa wenye dalili za Mpox zilipatikana mkoani Kagera, na kufikia Machi 9, 2025, serikali ilithibitisha rasmi uwepo wa wagonjwa wawili wa Mpox.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.