SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi milioni 720 kuanzisha shule mpya mbili katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma
Mkurugenzi wa Halmashari ya Wilaya ya Songea Neema Maghembe amezitaja shule hizo kuwa ni shule ya sekondari Kizuka katika Kata ya Kizuka ambayo serikali imetoa shilingi milioni 470 kutekeleza mradi huo.
Ameyataja majengo ambayo yanajengwa katika sekondari hiyo kupitia fedha za serikali za SEQUIP kuwa ni vyumba vinne vya madarasa,jengo la utawala,maktaba, vyoo na jengo la TEHAMA.
Amesema utekelezaji wa mradi huo hadi sasa umefikia asilimia 95 na kwamba shule inatarajia kuanza kuchukuwa wanafunzi kuanzia Januari 2023.
Mkurugenzi huyo pia ameitaja shule tarajiwa ya msingi inayojengwa katika kitongoji cha Lizaboni Kata ya Muhukuru iliyopo kilometa 140 kutoka mjini Songea ambayo serikali imetoa shilingi milioni 250 kutekeleza mradi huo.
“Mradi huu unatekelezwa na fedha kutoka serikali kuu kiasi cha shilingi milioni 250 ambazo zinajenga jengo la utawala,vyumba tisa vya madarasa na samani zake na vyoo matundu 30’’,alisema Maghembe.
Hata hivyo amesema mradi upo katika hatua za awali za utekelezaji na kwamba mradi unatarajiwa kukamilika Desemba 30 mwaka huu ambapo Januari mwakani shule inatarajia kuanza kuchukua wanafunzi.
Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki,ameipongeza Halmashauri hiyo kwa usimamizi unaofanywa kwenye miradi,hata hivyo ameagiza kuwa na mpango kazi wa kutembelea na kukagua miradi katika ngazi ya Halmashauri ili miradi iweze kutekelezwa kwa ubora na kwa wakati.
Ameagiza usimamizi unaofanywa kwenye miradi uheshimu kanuni za utawala bora,uwazi na ushirikishwaji na kwamba Halmashauri zijitahidi kuzijengea uwezo Kamati za Ujenzi ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na tija.
Imeandikwa na Albano Midelo
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Novemba 19,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.