SERIKALI kupitia wakala wa barabara za vijijini na mijini(Tarura),imeanza awamu ya kwanza ya ujenzi mradi wa barabara ya Longa- Kipololo-Litoho wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma yenye urefu wa km 1 kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi milioni 460.
Meneja wa TARURA wilaya ya Mbinga Mhandisi Oscar Mussa amesema,katika ujenzi wa barabara hiyo kazi zilizofanyika ni ujenzi wa tabaka mbili za lami,kujenga mitaro mita 300 na kufunga taa kumi za barabarani katika maeneo tofauti.
Aidha alisema,katika barabara hiyo wamejenga kipande kingine cha chenye urefu wa kilomita 25 kwa kiwango cha changarawe,na kuziba mashimo kwa gharama ya shilingi milioni 250.
Mhandisi Mussa alisema,mradi huo umetekelezwa na mkandarasi wa ndani kampuni ya Ovans Construction Ltd na ulianza kutekelezwa mwezi Agosti na kukamilika mwezi Disemba 2022,na sasa mkandarasi anakamilisha ujenzi wa mitaro.
Alisema,barabara hiyo ni muhimu sana kiuchumi kutokana na wananchi wengi wa maeneo hayo kuwa wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula na biashara hasa mahindi,kahawa na maharage ambapo sasa wataweza kusafirisha mazao yao kwenda sokoni kwa urahisi.
Mussa aliongeza kuwa,kujengwa kwa barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kuboreshwa kwa kiwango cha changarawe itarahisisha na kurudisha mawasiliano kati ya wilaya ya Mbinga na Nyasa na kufupisha safari kwa wananchi wa wilaya hizo mbili.
Amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza barabara hiyo na miundombinu yake, ili iweze kudumu kwa muda mrefu na iwasaidie katika shughuli zao za maendeleo kwa sababu fedha zilizotumika kufanikisha ujenzi huo zimetokana na kodi zao.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Litoho wilayani humo,wameshukuru kujengewa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani kwa muda mrefu walipata mateso makubwa pindi wanaposafiri kwenda Mbinga mjini ambapo walitumia kati ya masaa 4 hadi 6 na sasa wanatumia muda wa saa 1.
Hata hivyo Mapunda,ameiomba serikali kumalizia kipande kilichobaki cha barabara kujenga kwa lami badala ya changarawe,ili kuunganisha barabara mawasiliano kati ya wilaya ya Mbinga na Nyasa.
Gallus Hyera mkazi wa kijiji cha Ulima kata ya Ukata wilayani Mbinga alisema,kabla ya kujengwa kwa barabara hiyo kwa kiwango cha lami hali ya mawasiliano ilikuwa mbaya sana kwani wakati wa masika walilazimika kulala barabara kutokana na magari waliyokuwa wanasafiri nayo kukwama barabarani.Alieleza kuwa,hali hiyo imechelewesha saa maendeleo ya wananchi wa maeneo hayo licha ya kazi kubwa wanazozifanya za uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara.
Hyera,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoa fedha ambazo zimewezesha kujengwa kwa barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kuipongeza Tarura kwa kusimamia
ujenzi wa mradi huo muhimu kwa uchumi wa wilaya ya Mbinga.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.