Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza shilingi bilioni 93.2 kuboresha miundombinu ya bandari katika Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, hatua inayolenga kuimarisha usafiri wa majini na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa Ziwa Nyasa.
Uwekezaji huo umehusisha ujenzi wa bandari mpya ya Ndumbi kwa gharama ya shilingi bilioni 12.2, ambayo imekamilika na tayari imeanza kutoa huduma. Aidha, serikali imetenga shilingi bilioni 81 kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya kisasa ya Mbambabay unaotarajiwa kukamilika Januari 26, 2026.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya, amesema kuwa bandari ya Ndumbi imekamilika kwa asilimia 100 na inahudumia abiria na mizigo kwa ufanisi mkubwa. Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari za Ziwa Nyasa, Manga Gassaya, amesema bandari hiyo sasa ina uwezo wa kuhudumia mizigo ya hadi tani 110,000 kwa mwaka, kutoka tani 76,000 za awali, na abiria kutoka 56,000 hadi 126,000 kwa mwaka.
“Hii ni hatua kubwa katika kufungua usafirishaji wa ndani na nje ya nchi kupitia Ziwa Nyasa,” amesema Gassaya.
Kuhusu mradi wa bandari ya Mbambabay, Kaimu Mhandisi wa TPA, Fabian Paul, amesema bandari hiyo itakuwa na uwezo wa kupokea meli mbili zenye uzito wa tani 5,000 kila moja, jengo la utawala, ghala la kuhifadhi mizigo, nyumba za wafanyakazi na eneo la kuhudumia mizigo la mita za mraba 20,000.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, akizungumza alipotembelea kukagua mradi huo,alisema kukamilika kwa bandari hiyo kutaimarisha uchumi wa Mkoa wa Ruvuma na mahusiano ya kibiashara na nchi jirani za Malawi na Msumbiji.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.