Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka miwili imetoa Zaidi ya shilingi bilioni 244 kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Tunduru.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed wakati anazungumza na wananchi wa Tunduru kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Baraza la Eid mjini Tunduru.
Amesema fedha hizo zinaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya hiyo ikiwemo miradi katika sekta ya elimu ambapo hivi sasa katika wilaya hiyo wanafunzi wote wanaofaulu kujiunga na kidato cha kwanza wanachaguliwa kwa kuwa Wilaya ina miundombinu ya vyumba vya madarasa vya kutosha.
“Kwenye sekta ya afya napo tumepiga hatua kubwa kwani wananchi wetu wanapata huduma ya afya vizuri katika hospitali ya Wilaya,vituo vya afya na zahanati zetu kwa ukaribu zaidi’’,alisisitiza.
Akizungumzia sekta ya kilimo,Kanali Abbas amesema serikali imeimairisha mfumo wa stakabadhi za ghala ambapo wakulima wanauza mazao yao kwa bei ambayo inamwezesha mkulima kurudisha gharama zake anazozitumia katika uzalishaji.
Hata hivyo amesema karibu sekta zote zikiwemo za umeme,maji,barabara za vijijini na mjini zinafanya vizuri kutokana na serikali kutoa fedha za kutekeleza miradi hiyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Dr.Wilfred Rwechungura amesema Halmashauri hiyo inaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kukabiliana na upungufu wa madarasa ,madawati,viti na meza za wanafunzi.
Hata hivyo amesema hadi sasa katika shule za sekondari Halmashauri haina upungufu wa vyumba vya madarasa,viti na meza,badala yake kuna upungufu wa madarasa na madawati katika shule za msingi.
Rwechungura amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo,Halmashauri ya Wilaya imekuwa inatenga fedha kutoka vyanzo vya ndani na serikali kuu ili kujenga miundombinu ya shule ambapo kuanzia mwaka 2021 zaidi ya shilingi bilioni 2.5 zimetumika kujenga madarasa katika shule za msingi.
Kaimu Mkurugenzi huyo amesema kupitia mradi wa BOOST Halmashauri hiyo imeweza kupokea zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule za msingi.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma anafanya ziara ya kikazi katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma kwa lengo kuzungumza na wananchi ,kusikiliza kero zao na kupashana Habari za maendeleo zinazofanywa na serikali ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.