MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameagiza hekta 3500 zilizopo katika Shamba la NAFCO Namtumbo zitumiwe na Wakala wa Mbegu Tanzania ASA kuzalisha mbegu za serikali.
Ametoa agizo hilo katika kikao klichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo kilichowakutanisha Wakala wa Mbegu Tanzania (ASA),watalaam kutoka Halmashauri ya Namtumbo,Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya ya Namtumbo.
Hata hivyo amesema shamba lililokuwa na NAFCO Namtumbo ambalo Hazina imelikabidhi kwa ASA lina jumla ya hekta 5000 na kwamba hekta 1500 wameachiwa wananchi wa vijiji vya Suluti na Migelegele ili waweze kulima mazao mbalimbali.
“Nakuagiza Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo hakikisha wananchi wanasomewa hii barua kwamba shamba zima la NAFCO Namtumbo Hazina imelikabidhi rasmi kwa ASA,ili wananchi wajue mapema wasiingie kwenye mgogoro’’,alisisitiza Kanali Thomas.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma pia ameagiza shamba hilo litumike kuongeza mbegu za serikali hasa alizeti,ufuta na soya na mazao mengine yanayokubali katika ukanda za kusini.
Akizungumza kwenye kikao hicho Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu Tanzania (ASA) Dkt.Sophia Kashenge alisema serikali imeanisha shamba la NAFCO Namtumbo lenye ukubwa hekta 5000 liweze kutumika kuzalisha mbegu ili kuongeza uzalishaji wa mbegu nchini.
Amesema kikao kilichofanyika kati ya Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kimemaliza changamoto zilizojitokeza wakati wa uanishaji wa maeneo ya shamba hilo.
Hata hivyo Dkt.Kashenge amesema maelekezo ya Waziri wa Kilimo yalikuwa ni shamba la NAFCO Namtumbo litumike kuzalisha mbegu za serikali ili kukidhi mahitaji ya mbegu bora nchini.
Amesema serikali ilikuwa haina shamba la mbegu katika Kanda ya Kusini hivyo amesisitiza kuwa shamba hilo kwa upande wa serikali lina umuhimu mkubwa kwa ikolojia ya Kusini.
Amesisitiza kuwa serikali imeamua kuchukua shamba la NAFCO Namtumbo kama ilivyochukua shamba la NAFCO Mbozi ambalo hivi sasa lina jumla ya Kampuni nane zinazozalisha zaidi ya tani 7,000 za Mbegu.
Amesema shamba la NAFCO Namtumbo likitumika vizuri litaongeza mchango wa uzalishaji wa mbegu za serikali nchini.
Shamba la NAFCO Namtumbo lilikuwa chini ya Hazina,ambapo Msajiri wa Hazina amelikabidhi rasmi shamba hilo kwa Wakala wa Mbegu Tanzania(ASA).
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Desemba 2,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.