WAKAZI wa kijiji cha Ruvumachini Halmashauri ya mji Mbinga mkoani Ruvuma,wameishukuru serikali kwa kuanza ujenzi wa mradi mkubwa wa maji unaokwenda kumaliza kero ya muda mrefu ya maji safi na salama katika kijiji hicho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas walisema, tangu Serikali ilipoanza kujenga mradi huo wana matumaini makubwa ya kuishi na kuwa na maisha bora na kuondokana na tabu na mateso makubwa yanayo sababishwa na ukosefu wa maji ya bomba.
Akiongea kwa niaba ya wenzake Hagapi Komba alisema,changamoto ya maji katika kijiji hicho ni kubwa na ya muda mrefu hali iliyosababisha baadhi ya watumishi wa serikali wanaopelekwa kufanya kazi wakiwamo walimu wa shule ya msingi kuomba uhamisho kwenda shule nyingine na wengine kukimbia ili kuepuka kero ya maji.
Aidha alieleza kuwa,hata wanafunzi wanalazimika kwenda shule wakiwa wachafu,hivyo kusababisha kufanya vibaya katika masomo yao na kuiomba serikali kukamilisha mradi huo haraka.
Diwani wa kata ya Mpepai Donalt Mbepera, ameipongeza serikali kupitia wakala wa maji safi na salama vijijini(Ruwasa)mkoa waRuvuma kwa kuona umuhimu wa kujenga mradi huo ambao utahudumia wananchi wa kijiji hicho na vijiji vingine vinavyounda kata ya Mpepai.
Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Jonas Mbunda,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya kuhakikisha wananchi wa jimbo hilo wana kuwa na maisha bora kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali.
Mbunda alisema, uamuzi wa serikali kutoa kiasi cha Sh.bilioni 1.3 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo imethibitisha uaminifu wake kwa wananchi wa jimbo hilo na kudhihirisha kauli mbiu ya kumtua mama ndoo kichwani.
Amewaomba wananchi wa Ruvumachini na jimbo lote la Mbinga Mjini,kuhakikisha wanakuwa walinzi wa mradi huo na miradi mingine inayotekelezwa katika vijiji mbalimbali yenye lengo la kuleta maendeleo na kuboresha maisha yao.
Naye Mkuu wa mkoa huo Kanali Laban Thomas,ameuagiza uongozi wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira(Ruwasa) mkoa wa Ruvuma, kuhakikisha inamsimamia mkandarasi anayejenga mradi huo kampuni ya Nipo Africa Engineering ili akamilishe kazi kwa wakati na ubora wa hali ya juu.
Kanal Laban,amewataka wananchi wa kijiji cha Ruvuma chini,kutunza mradi huo pamoja na vyanzo vya maji na kuacha kufanya shughuli yoyote kwenye maeneo yaliyotengwa mahususi kwa ajili ya manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
Alisema,serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inafanya jitihada kubwa za kutafuta fedha ili kuboresha maisha ya wananchi wake,hata hivyo haitakuwa na maana iwapo miradi hiyo itahujumiwa na kutotaleta tija iliyokusudiwa.
Mkuu wa mkoa,amewakumbusha viongozi wa serikali ya kijiji na kata, kuhusu wajibu wao katika kusimamia vyanzo vya maji na kutumia sheria zilizopo kuwachukulia hatua watu wanaoharibu kwa makusudi vyanzo hivyo na miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Awali meneja wa Ruvuma wilaya ya Mbinga Mashaka Sinkara alisema,mradi wa maji wa Ruvuma chini ulianza kutekelezwa mwezi Machi mwaka huu na unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba.
Alisema,muda wa utekelezaji wa mradi huo ni miezi sita ambapo hadi sasa umefikia asilimia sitini na serikali imetenga Sh.bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo na unatarajiwa kuwanufaisha wakazi zaidi ya elfu moja.
Katika hatua nyingine Sinkara alieleza kuwa, serikali imetoa jumla ya Sh.bilioni 1.3 kwa ajili ya kujenga mradi mwingine wa maji Mbangamao kijiji cha Mbangamao chenye wakazi wapatao elfu mbili na mia tisa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.