.WAKULIMA wa zao la korosho wa mikoa ya Mbeya,Njombe na Ruvuma wanaohudumiwa na Chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma(Tamcu),wamevuka lengo la uzalishaji wa zao hilo katika msimu wa kilimo 2023/2024.
Ni baada ya kufanikiwa kuzalisha na kuuza jumla ya tani elfu 26.066 sawa na kilo milioni 26,066,333 zenye thamani ya Sh.bilioni 45,531,514,557 sawa na ongezeko la tani 1,000 ikilinganisha na msimu uliopita ambapo walizalisha kiasi cha tani 25,000.
Kaimu meneja wa Tamcu Marcelino Mrope amesema hayo jana,wakati akizungumza na wanachama wa chama cha msingi cha Ushirika Ligunga(Ligunga Amcos) katika mnada wa nane na wa mwisho katika msimu wa kilimo 2023/2024.
Mrope alisema,hayo ni mafanikio makubwa kwa wakulima na Chama hicho katika uzalishaji wa korosho ambapo amewapongeza wakulima kwa kazi nzuri waliyoifanya mashambani kwa mwaka 2023/2024.
Ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pembejeo za kilimo bure kwa wakulima, hali iliyohamasisha wakulima wengi kurudi mashambani kwa ajili ya kufufua mashamba yao.
“kwa mfano katika msimu huu wa kilimo 2024/2025 tumepewa pembejeo zenye thamani ya Sh.bilioni 22.5 kitu ambacho hakijawahi kutokea tangu nchi ipate Uhuru,tunaamini pembejeo hizi zitakwenda kuongeza sana uzalishaji wa korosho katika wilaya yetu”alisema Mrope.
Amewashauri wakulima kutumia vizuri fedha walizopata kununua pembejeo na kutumia mvua zilizoanza kunyesha kuanza maandalizi ya msimu mpya wa kilimo 2024/2025.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAMCU Mussa Manjaule alisema,bei ya korosho katika msimu wa mwaka huu haikuwa nzuri ikilinganisha na msimu uliopita,hata hivyo amewataka wakulima kutokatishwa tamaa badala yake waendelee kulima zao hilo ambalo ni nguzo kuu ya uchumi wao na wilaya ya Tunduru.
Manjaule,ametoa ushauri wake kwa wakulima kuanza kulima mazao mengine ya chakula na biashara ikiwemo zao maarufu la mbaazi ambalo lina soko la uhakika na bei kubwa na halihitaji gharama kubwa katika uzalishaji wake.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.