WAKALA wa barabara za mijini na vijijini Tanzania(TARURA)umeanza ujenzi wa barabara ya Islamic Center-Mkunguni kata ya Masonya Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma yenye urefu wa kilomita 1.7 kwa kiwango cha lami.
Ujenzi wa barabara hiyo,utasaidia kurudisha mawasiliano kwa wakazi wa mitaa ya Mkunguni na Misufini kwenda maeneo, kufuatia kuharibika kwa barabara za awali kutokana na mvua za masika zilizonyesha mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu.
Kaimu Meneja wa Tarura wilayani Tunduru Mhandisi Msolwa Julius amesema,mradi huo ni wa mwaka 2022/2023 wenye lengo la kuboresha mji wa Tunduru kwa barabara za lami ambapo utaigharimu serikali Shilingi milioni 769.
Msolwa alitaja muda wa ujenzi barabara hiyo ni siku 120,na imeanza kujengwa mwezi Januari na inatarajiwa kukamilika mwezi April mwaka huu na inatekelezwa na mkandarasi M/S Luke Associate Ltd chini ya usimamizi wa Tarura.
Amesema,kwa sasa kazi inazofanyika ni kutengeneza(kuseti) barabara yenyewe kabla ya kuweka vifusi na hatimaye kumwaga tabaka la lami kazi ambayo inayoendelea vizuri.
Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Said Bwanali,amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya kimkakati katika wilaya hiyo ikiwemo barabara hiyo na barabara ya Bias-Ikulu ndogo zinazojengwa kwa kiwango cha lami kuzingatia ubora,viwango na kukamilisha kwa wakati.
“barabara hizi za lami na zile zinazojengwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya yetu ya Tunduru tunataka zikamilike kwa muda uliopangwa,dhamira ya serikali yetu ya awamu ya sit ani kusogeza huduma kwa wananchi na siyo vinginevyo”alisema Bwanali.
Bwanali ambaye ni diwani wa Masonya,ameishukuru serikali kwa kuendelea kuitengea fedha Tarura kwa ajili ya kujenga barabara za lami katika mji wa Tunduru na kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Alisema wilaya ya Tunduru ni kongwe hapa nchini, na maendeleo yanayofanyika sasa walizoea kuyaona katika mikoa mingine hapa,lakini tangu serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani miaka miwili imefanya mambo mengi na mazuri ya maendeleo ambayo yamebadilisha muonekano na maisha ya wakazi wa Tunduru.
Alisema,barabara ya Islamic Center-Mkunguni ilikuwa haipitiki kirahisi kutokana na kuharibika vibaya na mvua zinazoendelea kunyesha na ameipongeza Tarura kwa kazi nzuri ya kutekeleza na kusimamia ujenzi wa barabara katika wilaya hiyo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.