SHIRIKA la Kikristo la Compassion International Tanzania (CIT) lililojikita kuwasaidia Watoto wanaotoka kaya masikini limeweza kuwahudumia Watoto 4200 katika Mkoa wa Ruvuma.
Hayo yamesema na Mkurugenzi wa CIT nchini Mary Lema wakati anazungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya ulinzi wa mtoto iliyofanyika katika viwanja vya kanisa la Anglikana Kijiji cha Mkongo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.
Lema amesema Shirika la CIT liliingia mkoani Ruvuma mwaka 2019 na kuanza kutoa fedha za ufadhili kwa Watoto kutoka kaya masikini Machi mwaka 2020.
“Matokeo ya huduma hii yamekuwa Dhahiri kwa ukubwa wake kwa Watoto walengwa,walezi,kaya na jamii kwa ujumla, kwa kushirikiana na makanisa,tumeweza kuboresha mazingira ya elimu kwa Watoto kwa kuhakikisha wanapata mahitaji wezeshi kama vitabu,sare za shule na kutoa Bima ya afya’’,alisisitiza Mkurugenzi wa CIT.
Hata hivyo amesema Shirika la CIT kwa kushirikiana na makanisa wenza, wanaweza kuhudumia Watoto na vijana katika Nyanja mbalimbali za Maisha huku mkazo mkubwa ukiwekwa kisera na kivitendo ili kuhakikisha mtoto analindwa dhidi ya vitendo vya unyanyasaji.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa CIT,Shirika hilo lilianza kufanya kazi hapa nchini mwaka 1999 jijini Arusha ambapo hivi sasa linafanya kazi katika mikoa 21 na wilaya 80 na kwamba hadi sasa limefadhili Watoto na vijana walengwa Zaidi ya 112,000 kupitia makanisa washirika Zaidi ya 503.
Mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo,Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Godwin Rutta amelipongeza Shirika hilo kwa kazi kubwa inayoendelea kufanywa kwa wananchi bila ubaguzi wowote.
Amesema serikali inatambua mchango huo na ipo tayari wakati wowote kushirikiana na makanisa ili kuhakikisha nia njema iliyokusudiwa ya kuboresha maisha inawafikia wananchi.
Ametoa rai kwa wananchi wa madhehebu yote wilayani humo kuhakikisha wanawapeleka Watoto wao kupata elimu katika shule inayomilikiwa na kanisa la Anglikana ili kuwajengea Watoto wao msingi wa elimu.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo Naibu Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma padre Martin Mande amelipongeza Shirika la CIT kwa kusaidia huduma ya mtoto katika kanisa hilo.
“CIT mmetufanya kanisa lionekane linafanya kazi yake kimwili na kiroho kwa ufanisi mkubwa,mmetembelea Ruvuma na kufika hapa Mkongo kwenye kituo cha Anglikana sisi hatukuwa hivi tunawashukuru sana’’,alisisitiza Naibu Askofu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Ruvuma,Padre John Midelo amesema mradi huo umeweza kumkomboa mtoto katika umasikini.
Hata hivyo amesema mradi unatekelezwa katika makanisa yaliyopo wilaya za Namtumbo,Tunduru na Songea wanufaika wakubwa ni Watoto na vijana wanaotoka katika kaya masikini.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu kanisa la serikali wamenufaika kupitia mradi huo ambapo kanisa Anglikana pekee limeajiri vijana 23 na Watoto wengi wakinufaika na uwepo wa shule zinazoendeshwa kupitia mradi huu ambapo katika kituo cha Mkongo wanatarajia kukamilisha usajiri wa shule hiyo hivi karibuni.
Imeandikwa na Albano Midelo
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Julai 7,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.