SERIKALI kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kuongeza Wanyama jamii ya simba, chui, fisi,mbuni,kobe na mamba katika bustani ya wanyamapori Luhira Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma
Antony Masebe ni Kamanda wa Kituo Kidogo cha Kanda Kusini Mashariki amesema utengenezaji wa vibanda maalum vya kuwahifadhi Wanyama hao (cages) unaogharimu shilingi milioni 78 unaendelea katika bustani ya Luhira.
Masebe amesema serikali pia imetoa shilingi milioni 103 kujenga ukumbi wa kisasa katika bustani hiyo na vibanda viwili vya kupumzikia ambavyo vimegharimu shilingi milioni 20.
Amesema kituo hicho ambacho kipo chini ya TAWA kinasimamia bustani ya asili ya Luhira ambayo ilianzishwa mwaka 1973 na imekuwa inapokea watalii wa aina mbalimbali kutoka ndani ya nje ya nchi.
“Bustani ya Luhira imekuwa inatoa elimu na kuwasaidia wanafunzi kuanzia shule za msingi,sekondari na vyuo kuweza kujipatia maarifa tofauti kuhusu utalii ’’,alisisitiza Masebe.
Daudi Tesha ni Afisa Mhifadhi katika Bustani ya Luhira ameitaja bustani hiyo kuwa ndiyo bustani pekee Tanzania yenye uoto wa asili ikiwa na ukubwa wa hekta 600 ipo umbali wa kilometa saba kutoka mjini Songea.
Amewataja Wanyama ambao wanapatikana katika bustani hiyo kuwa ni pundamilia, pofu, kakakuona, kuro, swalapala, sungura,nyumbu,jamii ya nyani ambapo amesema bustani hiyo ina madhari ya kuvutia ikiwemo maeneo ya michezo ya Watoto,maeneo mazuri ya kupigia picha na kuweka kambi kwa ajili ya utafiti.
Amekitaja kiingilio cha bustani hiyo kuwa ni shilingi 2,360 kwa mtu wa kuanzia umri wa miaka 18,chini ya miaka 17 ni shilingi 1180 na kwa Watoto chini ya miaka mitano wanaingia bure hivyo ametoa rai kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma na watanzania wote kutembelea bustani hiyo asili.
Amesema bustani ya Luhira imeweka mkakati wa kuwa na aina mbili za makazi ya Wanyama wakiwemo Wanyama huru kama pundamilia na pofu na kwamba hivi sasa wanatarajia kuongeza Wanyama wanaishi kwenye vizuizi yaani cages ambapo mpango uliopo ni kuleta Wanyama wanaovutia wengi kama mfalme wa msituni simba na chui.
“Hifadhi ya Luhira ina eneo kubwa, ambalo linahitaji uwekezaji mkubwa,tunafikiria kuwaleta wanyama wakubwa kama simba na kuongeza maeneo ya kuvutia wageni wanapokuwa ndani ya bustani ya Luhira’’,alisisitiza Tesha.
Ameitaja mikakati mingine ya kuboresha bustani hiyo kuwa ni kuanzisha michezo ya kutekeleza kwenye waya (Zipline) kama inavyofanyika katika nchi ya Afrika ya Kusini,kuweka bwawa la kisasa la kuogelea na kuboresha eneo maalum la kupigia picha.
Amesema baada ya kuoresha bustani hiyo na kuongeza vivuito wanatarajia pia idadi ya watalii kutoka ndani na nje pia itaongezeka.
Ametoa rai kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma na mikoa ya kusini kufika katika hifadhi ya Luhira kujionea fursa za utalii zilizopo katika hifadhi hiyo pekee ya asili nchini Tanzania iliyopo mjini Songea.
Tesha amesisitiza kuwa hifadhi ya Luhira ni eneo la asili lenye utajiri wa miti ya miyombo, misuku, mitumbitumbi, miwanga, minyonyo, mizambarau, mininga, na mikuyu,na kwamba ni miongoni mwa bustani chache zenye uoto wa asili kabisa zilizopo mjini.
Amesema ndani ya Luhira,mtalii anaweza kufanya utalii wa kutembea kwa miguu,kupiga picha,kuangalia wanyama na ndege,utalii wa kuweka kambi(camping) na kwamba mapumziko ya mchana(picnic) hufanyika ndani ya eneo maalum katika bustani hiyo.
“Watalii kutoka nje ya nchi pia wanatembelea hifadhi yetu, tumepokea watalii toka Ujerumani,Afrika ya Kusini, India, Marekani, Ufaransa,Italia, Uholanzi na wageni toka mikoa mbalimbali nchini,wanafanya utalii wa kuchunguza aina ya mimea na ndege’’,alisema Tesha.
Hifadhi ya asili ya Ruhila,inafikika kwa urahisi kwa ndege au kutumia barabara ya Njombe hadi Songea,Mtwara hadi Songea ambayo ni ya lami.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Desemba 9,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.